1 Septemba 2025 - 08:50
Source: Parstoday
Hamas: Wito wa Smotrich wa kuwaua watu wa Gaza kwa njaa na kiu ni kukiri mauaji ya kimbari

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kuwa, wito uliotolewa na Waziri wa Fedha wa Israel mwenye itikadi kali, Bezalel Smotrich, wa kukata maji, umeme na usambazaji wa chakula katika Ukanda wa Gaza ni kukiri wazi sera za utawala huo vamizi za kutenda mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.

Harakati hiyo imesisitiza katika taarifa yake, kwamba matamshi ya Smotrich yanawakilisha mwito uliotangazwa wa kuendeleza uhalifu wa jeshi la utawala ghasibu huko Gaza hadi watu wetu waangamizwe au kuyahama makazi yao. Pia yanawakilisha kukiri rasmi kwa matumizi ya njaa na kuzingirwa raia wasio na hatia kama silaha, suala ambalo ni uhalifu wa kivita.

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa yaliyosemwa na Bezalel Smotrich yanajumuisha kukiri wazi kwa mradi wa kuwalazimisha Wapalestina kuhama nchi yao na maangamizi ya kizazi dhidi ya taifa letu, na ni ushahidi tosha wa kuhukumiwa utawala vamizi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na Mahakama ya Kimataifa ya Haki, kwa kuzingatia nia ya viongozi wa utawala wa kifashisti ya kutekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari.

Hamas imesisitiza kuwa kauli ya Smotrich si maoni ya mtu binafsi mwenye msimamo mkali, bali ni sera ya serikali iliyotangazwa ambayo inatekelezwa kwa karibu miezi 23 sasa, ikiwa ni pamoja na kuwanyima chakula na dawa Wapalestina, kulipuliwa kwa vituo vya misaada ya kibinadamu, uharibifu wa miundombinu, na jitihada za kuwalazimisha watu kukimbia makazi yao.

Hamas imeeleza kuwa matamshi hayo yanafichua dhati halisi ya utawala wa Israel na kuthibitisha kwamba kinachotokea Gaza ni mradi wa mauaji ya kimbari na kulazimisha watu kuyahama makazi yao, jambo ambalo linahitaji hatua za haraka za kimataifa za kuwawajibisha viongozi wake.

Mapema siku ya Alhamisi, Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich alitoa wito wa kuzingirwa kikamilifu mji wa Gaza na kambi za wakimbizi za katikati mwa Ukanda wa Gaza, na kuwaua wapiganaji wa Hamas kwa njaa na kiu, na baadaye kulinyakua eneo lote la Ukanda wa Gaza.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha