Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa majeshi ya Yemen, ametangaza kupitia taarifa ya televisheni siku ya Jumatatu kuwa majeshi ya Yemen yamefanya shambulio dhidi ya meli ya Scarlet Ray, iliyokuwa na bendera ya Liberia, katika ncha ya kaskazini ya Bahari ya Sham. Shambulio hilo limetekelezwa kwa kutumia kombora la balistiki la kupiga meli (ASBM) lililotengenezwa nchini Yemen.
Jenerali Saree amesema operesheni hiyo imefanikiwa kwa kiwango cha juu, kwani kombora hilo lililenga moja kwa moja meli hiyo na kufanikisha malengo ya kijeshi yaliyokusudiwa.
Amesisitiza kuwa majeshi ya Yemen "yataendelea kuunga mkono watu wa Palestina kwa kuzuia meli za Israel kupita katika Bahari ya Sham na Bahari ya Arabuni, wakati zikielekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu."
Aidha, amesema vitengo vya jeshi la Yemen vitaendeleza operesheni zao hadi mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yakome na mzingiro wa eneo hilo uondolewe.
Kama sehemu ya kujibu mauaji yanayoendelea kufanywa na Israel huko Gaza tangu Oktoba 2023, Yemen ilianzisha vikwazo vya kimkakati vya baharini ili kuzuia mtiririko wa vifaa vya kijeshi kuelekea Israel. Viongozi wa Yemen pia wamehimiza jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kushughulikia mgogoro mkubwa wa binadamu unaoendelea Gaza.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Yemen imeongeza shughuli zake katika Bahari ya Sham, ikiendelea kushambulia meli zinazohusiana na Israel katika njia muhimu za baharini.
Mnamo Agosti 6, serikali ya Yemen ilitangaza vikwazo dhidi ya wamiliki wa meli 64 waliokuwa wakikiuka vizuizi vya baharini. Meli hizo zimepigwa marufuku kupita katika Bahari ya Sham, mlango wa Bab al-Mandab, Ghuba ya Aden, na Bahari ya Arabuni. Serikali imeonya kuwa vyombo hivyo vitashambuliwa iwapo vitapatikana ndani ya maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya Yemen.
Mnamo Julai, majeshi ya Yemen yalishambulia na kuzamisha meli mbili—Eternity C na Magic Seas—zilizokuwa zikielekea Israel kupitia Bahari ya Sham.
Kati ya Novemba 2023 na Januari 2025, Yemen imefanya zaidi ya operesheni 100 dhidi ya meli zinazohusiana na Israel, hatua ambayo imeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa hilo.
Majeshi ya Yemen yameeleza wazi kuwa operesheni hizo zitaendelea hadi Israel itakapositisha mashambulizi ya ardhini na ya angani dhidi ya Gaza.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa zaidi ya Wapalestina 63,400 wameuawa huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Your Comment