3 Septemba 2025 - 23:40
Source: Parstoday
‘Majibu ya awali’: Yemen yatekeleza mashambulizi ya makombora dhidi ya Tel Aviv, uwanja wa ndege wafungwa

Jeshi la Yemen limetekeleza mashambulizi ya makombora dhidi ya Tel Aviv, hatua iliyosababisha kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion na kuwalazimu Waisraeli kukimbilia usalama kwenye mahandaki.

Katika tamko lililotolewa Jumatano, jeshi la Yemen limesema limefanya operesheni ya kijeshi ya kipekee yenye hatua mbili kwa kutumia makombora mawili ya balestiki: “Palestine-2” na “Zulfiqar.”

Shambulizi hilo limetajwa kama hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya kampeni ya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala wa Israel huko Gaza. Aidha operesheni hiyo imetajwa kuwa “majibu ya awali” ya uchokozi wa Israel dhidi ya Yemen.

Shambulizi la anga la Israel lililolenga mji mkuu wa Yemen Alhamisi iliyopita lilisababisha vifo vya Waziri Mkuu Ahmed Ghaleb Al-Rahawi wa Serikali ya Kitaifa ya Mabadiliko na Ujenzi, pamoja na maafisa wengine wanane. Licha ya madai ya jeshi la Israel kwamba lilidhibiti shambulizi hilo, kombora hilo lilisababisha usumbufu mkubwa wa shughuli, ikiwemo kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion na kusikika ving'ora katika mkoa wa Tel Aviv.

Kwa mujibu wa tamko hilo, makombora hayo “yalilenga maeneo nyeti ya adui wa Israel katika eneo la Yaffa linalokaliwa kwa mabavu.” Tamko hilo liliongeza kuwa: “Operesheni hiyo imefanikiwa kutimiza malengo yake, na kusababisha mamilioni ya Wazayuni maghasibu kukimbilia kwenye mahandaki, na kusimamisha shughuli za uwanja wa ndege.”

Aidha, tamko hilo limeeleza kuwa Israel inatenda “uovu mkubwa dhidi ya Waislamu milioni mbili huko Gaza, ardhi ya jihadi na shahada, huku ulimwengu wa Waislamu bilioni mbili ukikaa kimya bila kuchukua hatua.” Jeshi la Yemen limesisitiza kuwa “adui Muisraeli" hatafurahia usalama na utulivu, na kwamba operesheni za Yemen zitaendelea kwa kasi inayoongezeka katika kipindi kijacho.”

Tangu kuanzishwa kwa vita vya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023, vikosi vya Yemen vimefanya mashambulizi kadhaa kuonesha mshikamano na Wapalestina, vikilenga viwanja vya ndege, bandari na maeneo mengine chini ya utawala wa Israel.

Yemen imeahidi kuwa mashambulizi haya yataendelea almradi vita na vizuizi dhidi ya Gaza vinaendelea. Vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 63,600 na majeruhi zaidi ya 160,900, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha