Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Jeshi la Israeli limetangaza asubuhi ya leo Ijumaa kuwa ndege zake za kivita zimefanya mlolongo wa mashambulio ya anga dhidi ya malengo katika kusini mwa Lebanon. Kulingana na madai ya Tel Aviv, mashambulio haya yalilenga vituo vilivyotumika na Hezbollah kusimamia mifumo ya moto na ulinzi.
Msemaji wa jeshi la Israeli alisema kuwa katika operesheni hii ziliharibiwa silaha, majengo ya kijeshi na miundombinu ya chini ya ardhi ya Hezbollah. Wakati huo huo, video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha kuwa baadhi ya mashambulio yalighusisha pia mikahawa na ukumbi wa harusi karibu na mji wa Nabatieh.
Vilevile, usiku wa Alhamisi, jeshi la Israeli lilitangaza kuua wanachama watatu wa Hezbollah kusini mwa Lebanon. Kulingana na vyombo vya habari vya Israeli, mmoja wa waliouawa alikuwa Ali Muhammad Qarouni, aliyedaiwa kuwa mwakilishi wa Hezbollah katika eneo la Kafra na alikuwa akishughulikia uratibu wa kiuchumi na kijeshi wa chama hicho katika eneo hilo.
Jeshi la Israeli linasema kuwa Qarouni alitumia nyumba za kukodi kuhifadhi silaha na kufanya operesheni za ufuatiliaji. Wengine wawili, Ahmed Saad na Mustafa Rizq, waliuawa katika shambulio jingine katika eneo la Kafr Raman. Wao walidaiwa kuwa wahandisi wa Hezbollah waliokuwa wakishirikiana katika ujenzi upya wa miundombinu ya kijeshi katika maeneo ya Jabal Dof na Al-Khiyam.
Hadi sasa, Hezbollah Lebanon haijatoa kauli rasmi kuhusu ripoti za Israeli za kuuliwa kwa wanajeshi wake. Harakati hii mara nyingi hujibu kwa kuchelewa au mara nyingine bila taarifa rasmi.
Tangu mwisho wa Novemba mwaka jana, mapigano ya mpaka kati ya Hezbollah na jeshi la Israeli yameongezeka, na mashambulio ya anga na ndege zisizo na rubani ya Israeli katika kusini mwa Lebanon yanaendelea karibu kila siku. Jeshi la Israeli linaendelea kudhibiti pointi tano za mpaka katika kusini mwa Lebanon. Tel Aviv na Washington wameitaka Hezbollah iweke silaha chini, lakini ombi hilo linakabiliwa na upinzani ndani ya Lebanon.
Your Comment