Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (AS) –ABNA– Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hujjatul-Islam Gholam-Hossein Mohseni Ejei, amesema kuwa madai ya Marekani ya kutetea haki za binadamu hayawezi kuaminika na ni ya kichekesho kutokana na historia ya vitendo vya Marekani dhidi ya watu wa Iran na mataifa mengine duniani.
Akizungumza wakati wa kuanza kwa "Wiki ya Haki za Binadamu za Marekani", inayokumbusha kile Iran inachokieleza kuwa ni uhalifu wa kibinadamu uliofanywa na utawala wa Marekani dhidi ya wananchi wa Iran na mataifa mengine, Mohseni Ejei alisema kuwa miongoni mwa nyenzo za utawala wa Marekani katika kutekeleza sera zake za kiutawala ni pamoja na mashambulizi ya kijeshi, ugaidi wa kiuchumi na vita vya vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Idara ya Mahakama ya Iran, Mohseni Ejei alieleza kuwa Marekani imebobea katika kupindisha ukweli, kuonesha batili kana kwamba ni haki na kuficha au kusafisha sura ya uhalifu wake kupitia propaganda za kimataifa.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mahakama ya Iran aliwapokea wajumbe wa Kamati Kuu ya "Wiki ya Kusoma Upya na Kufichua Haki za Binadamu za Marekani", akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuanika rekodi ya Marekani katika masuala ya haki za binadamu na kuwafahamisha watu wa dunia kuhusu madhara ya sera zake.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa taasisi za kielimu, vyombo vya habari na wanaharakati wa haki za binadamu kuendelea kufichua ukweli na kupambana na kampeni za upotoshaji zinazolenga kuficha uhalisia wa matukio ya kimataifa.
Your Comment