Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) –ABNA– Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Fatemeh Mohajerani, amesema kuwa taifa la Iran lina deni la milele kwa watoto waliopoteza maisha katika tukio la Minab, akisisitiza kuwa kumbukumbu yao itaendelea kuishi katika nyoyo za wananchi.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mohajerani alikuwa ameshika tasbihi mkononi, akieleza kuwa aliikabidhiwa na mama mmoja wa shahidi wa Minab ambaye aliibariki tasbihi hiyo katika mji mtukufu wa Karbala na kumuomba waendelee kumkumbuka mwanawe aliyefariki shahidi.
Mohajerani alisema ni wajibu wa taifa kuwakumbuka watoto ambao maisha yao yalikatishwa kabla ya kutimiza ndoto zao. Alitaja kwa masikitiko watoto waliokuwa katika shule ya awali na madarasa ya mwanzo, akieleza simulizi ya baba mmoja aliyemtambua mtoto wake kupitia soksi alizokuwa amevaa asubuhi ya siku ya tukio.
Aidha, alisisitiza kuwa Iran haitawasahau watoto hao, akisema kuwa wamekuwa sehemu ya historia na utukufu wa taifa, huku akiombea Iran iendelee kusimama imara na yenye heshima milele.
Maoni yako