19 Machi 2011 - 20:30

Waziri wa Sheria wa serikali ya mpito ya Libya amesema kuwa Seiful Islam, mwana wa aliyekuwa dikteta wa Libya Muammar Gaddafi amekamatwa karibu na mji wa Obari, magharibi mwa mji wa milima wa Zintan.

Muhammad al Alagy amesema kuwa, Seiful Islam Gaddafi amekamatwa na vikosi vya wanamapinduzi na kwamba hajapata majeraha yoyote katika operesheni ya kumsaka. Taarifa ya Baraza la Mpito la Libya imeongeza kuwa, mwana huyo wa aliyekuwa dikteta wa Libya aliyeuawa, amekamatwa pamoja na walinzi wake watatu na kwamba, hatua hiyo ni mafanikio mengine kwa Walibya na harakati zao za kutaka kuelekea katika demokrasia halisi. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa waranti wa kukamatwa Seiful Islam, babake Muammar Gaddafi na Abdullah al Sennusi, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Kiintelijensia wa utawala wa Gaddafi, kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu.
Kanali Muammar Gaddafi, dikteta aliyeongoza Libya kwa ngumi ya chuma kwa zaidi ya miongo minne aliuawa mwezi mmoja uliopita katika mji alikozaliwa wa Sirte baada ya kukamatwa na askari wanamapinduzi