19 Machi 2011 - 20:30

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema istiqama na msimamo thabiti wa taifa la Iran mbele ya madhalim na wakoloni ni matunda na baraka za Mapinduzi ya Kiislamu.

ABNA inatuhabarisha kuwa:Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya makamanda na wakuu wa jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuasisiwa kwa jeshi hilo na kusisitiza kuwa kwa baraka za izza ya nafsi walizopata kutokana na Mapinduzi ya Kiislamu wananchi na viongozi wa Iran wameweza kusimama imara kukabiliana na wasitikbari na wakoloni na kuivunja irada ya maadui.Kiongozi Muadhamu ameashiria pia rekodi chafu ya madola ya kikoloni na hasa Uingereza katika kuyadhalilisha mataifa na kufuta turathi zao za kihistoria sambamba na kujenga hisia za kujiona dhaifu na kutokuwa na uwezo ndani ya mataifa hayo ili kuweza kuyadhibiti na kuyatia mkononi maliasili na utajiri wao na akabainisha kuwa katika enzi za tawala za Qajar na Pahlavi nchini Iran viongozi walikuwa dhalili na dhaifu katika kukabiliana na matakwa ya mabeberu, na kwa sababu hiyo wakashindwa kuchukua hatua chanya na za maana kwa maslahi ya taifa la Iran. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa wananchi wa Iran wanapaswa kuienzi thamani ya izza waliyotunukiwa na Mapinduzi ya Kiislamu. Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi ametoa nasaha pia kwa vikosi vya majini vya jeshi na vya jeshi la walinzi wa Jamhuri ya Kiislamu za kuvitaka vilipe uzito na umuhimu maradufu suala la utekelezaji wa majukumu yao sambamba na kuongeza na kuimarisha zaidi uwezo wao wa ustadi na umahiri wa aina mbalimbali, uwezo wa kielimu, azma, irada na kushikamana kwao na dini.