19 Machi 2011 - 20:30

Milipuko mitatu imeilenga miji miwili ya Kenya ya Mandera na Wajir katika mkoa wa Kaskazini Mashariki jirani na Somalia ambapo taarifa za awali zinasema, polisi mmoja ameuawa na wengine kumi kujeruhiwa

Mashambulio hayo yaliyotekelezwa na wanamgambo wa ash Shabab yalivilenga vikosi vya usalama katika maeneo hayo. Leo Nyongesa, Mkuu Polisi katika mkoa wa Kaskazini Mashariki amelaani shambulio hilo na kuthibitisha kuuawa polisi mmoja. Taarifa zaidi zinasema mashambulio hayo ya wanamgambo wa ash Shabab yamezusha wasi wasi mkubwa kwa wakazi wa miji ya Mandera na Wajir. Hili sio shambulio la kwanza la bomu la wanamgambo wa ash Shabab wa Somalia. Tangu Kenya ilipotuma vikosi vyake vya kijeshi nchini Somalia kwa shabaha ya kupambana na wanamgambo wa ash Shabab katikati mwa mwezi Oktoba, Kenya imeshuhudia mashambulio kadhaa ya mabomu ya wanamgambo wa ash Shabab wanaodai kulipiza kisasi kwa hatua ya Nairobi ya kutuma vikosi vyake Somalia.