Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) wamemfariji Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha mumewe, Marehemu Hafidh Ameir Hassan.
Mwenyekiti wa JMAT Taifa, Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum, akiambatana na Katibu Mkuu wa JMAT Taifa, Askofu Dkt. Israel Maasa Ole Gabriel, pamoja na viongozi wengine wa jumuiya hiyo, walifika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, Septemba 11, 2026, kumpa pole Rais Samia na familia yake.
Marehemu Hafidh Ameir Hassan alifariki dunia Septemba 7, 2026, katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Zanzibar, ambako alikuwa akipatiwa matibabu. Baadaye alizikwa Kizimkazi, Kusini Unguja, katika mazishi yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na jamii.
Katika ujumbe wao wa pole, viongozi wa JMAT wameeleza kuwa wanaiunga mkono familia ya Rais Samia katika kipindi hiki cha majonzi, huku wakitoa dua kwa Mwenyezi Mungu awajalie subira, nguvu na faraja.
JMAT pia imesisitiza umuhimu wa amani, maridhiano, upendo na mshikamano wa kitaifa, hasa katika nyakati za majonzi zinazohitaji Watanzania kusimama pamoja na kupeana faraja.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Hafidh Ameir Hassan mahali pema peponi, na awape Rais Samia pamoja na familia yake subira na nguvu katika kipindi hiki kigumu. Amina.

Maoni yako