19 Machi 2011 - 20:30

Mkuu wa Baraza la Taifa la mpito nchini Libya ametetea hatua ya nchi hiyo ya kuwa mwenyeji wa Rais Omar Hassan Al-Bashir wa Sudan mjini Tripoli na kusema kuwa Khartoum iliwasaidia kwa hali na mali wanamapinduzi wa Libya hadi walipomuangusha dikteta wa zamani Kanali Muamar Gaddafi.

Matamshi ya Mustafa Abdul Jalil ni radiamali kwa matamshi yaliyotolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo shirika la Human Rights Watch ambalo mbali na kukosoa safari hiyo ya Rais Bashir, pia limewataka viongozi wa Tripoli kumtia mbaroni kiongozi huyo na kumkabidhi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Rais wa Sudan anawindwa na mahakama hiyo ya mjini Hague, Uholanzi kwa tuhuma za mauaji ya kimbari na ukiukaji wa haki za binadamu katika jimbo la Darfur. Rais Bashir amekanusha tuhuma hizo za ICC na kuzitaja kuwa za kipuuzi.