Kauli hiyo ya Lipumba ambaye pia ni kitaaluma ni mchumi imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Kamati za Bunge za Mashirika ya Umma (POAC), Serikali za Mitaa (LAAC) na ya hesabu za Serikali Kuu (PAC) kuwasilisha ripoti zake bungeni zinazoonyesha kukithiri kwa vitendo vya ufisadi serikalini na matumizi mabaya ya fedha za umma.Profesa Lipumba alisema ubadhilifu huo unaonyesha ni jinsi gani watendaji wa Serikali hawaheshimu na kufuata kanuni na sheria za matumizi ya mali za umma na hivyo wanapaswa kujiuzulu na kupelekwa mahakamani.Alisema wakati nchi ikihangaika na mfumuko wa bei na kuongezeka kwa ukali wa maisha unaowaumiza wananchi, bado taasisi nyingi za Serikali zinakwapua fedha za umma ambazo zingeweza kusaidia katika maendeleo mengine.“Utawala mbovu ni sababu kubwa inayochangia ubadhilifu huu kuendela katika taasisi nyingi za Serikali, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani watendaji wa Serikali hawaheshimu sheria zilizopo na wanapaswa kuwajibishwa haraka” alisema Lipumba na kuongeza:“Fedha hizo zinazoibiwa na watu wachache zingeweza kutumika katika sekta nyingi tu ambazo ziko katika hali mbaya ya ukosefu wa vifaa na vitendea kazi ikiwamo sekta ya elimu na afya ambazo zina changamoto kubwa”.Alisema kuwa matumizi mabaya ya Serikali yataipeleka nchi katika hatari kubwa ya kuyumba kwa uchumi wa nchi na ili kukabiliana na aibu hiyo ni lazima viongozi waliohusika kuwajibishwa.Alisema Serikali imeshindwa kusimamia na kuendeleza mipango na sera zake kutokana na kuwalinda watendaji wezi wanaoitia hasara Serikali kwa kujihusisha katika ufisadi wa fedha na mali za umma.
19 Aprili 2012 - 19:30
Msimbo wa Habari: 309968
Mwenyekiti wa (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameitaka Serikali kuwawajibisha Mawaziri na Watendaji wa Serikali waliohusika katika wizi wa fedha za umma kwakuwa jambo hilo linahatarisha mwenendo wa uchumi wa nchi.