5 Novemba 2012 - 10:34

Kwa mara ya kwanza Israeli imekiri kumuua aliyekuwa kiongozi namba mbili wa chama cha ukombozi cha Wapalestina-PLO, Abu Jihad katika shambulio lililofanywa katika makao makuu ya chama hicho mjini Tunis mwaka 1988.

ABNA-Taarifa iliyochapishwa na gazeti la Israeli la Yediot Aharonot , imeeleza kuwa operesheni hiyo ilipangwa na shirika la ujasusi la Israeli, Mossad na iliendeshwa na kikosi cha makomandoo cha Sayeret Matkal.

Operesheni hiyo iliamriwa na Nahum Lev, ambaye katika mahojiano kabla ya kifo chake mwaka 2000, alikiri kuhusika kwake katika operesheni hiyo, ingawa taarifa hiyo haikuchapishwa.

Abu Jihad, aliyekuwa rafiki wa muda mrefu na msaidizi wa kiongozi wa zamani wa PLO, Yasser Arafat, alishiriki kikamilifu katika kuongoza vuguvugu la maandamano ya upinzani- Intifada mwaka 1987 hadi 1994 dhidi ya makaazi ya Israeli.

Alul anasema wakati mauaji hayo yanafanyika Yitzhak Shamir, alikuwa Waziri Mkuu na Yitzhak Rabin akiwa waziri wa ulinzi, ambaye baadae alikuwa waziri mkuu hadi alipouawa na wapiganaji wa mrengo wa kulia mwaka 1995.

Taarifa hizo zinaonyesha kuwa makomandoo 26 wa Sayeret Matkal waliwasili kwenye ufukwe wa Tunis jioni ya Aprili 15, mwaka 1988 na kugawanyika katika makundi mawili na kusafirishwa hadi karibu na makaazi ya Abu Jihad.