19 Novemba 2012 - 17:02

Wapalestina 13 wamefariki leo katika Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga yanayofanywa na Israel, ambayo mpaka sasa yamesababisha jumla ya watu 86 kupoteza maisha tangu Israel ianze kufanya mashambulizi hayo kwenye Ukanda wa Gaza kwa siku sita mfululizo.

Shambulizi la mwisho lilifanywa saa 1 asubuhi kwa saa za huko, ambapo helikopta ya Israel ilishambulia gari moja, na kusababisha vifo vya watu watatu. Wakati huohuo, ndege za kijeshi za Israel aina ya F16 zilirusha mabomu dhidi ya nyumba tatu katika sehemu ya Al-Zeitoun karibu na mji wa Gaza, na kuua watu wanne, wakiwemo mtoto mmoja na wanawake wawili. Awali, mashambulizi ya Israel yalisababisha vifo vya wapiganaji watatu wa Kundi la Islamic Jihad, na raia wengine watatu wa Palestina.

Habari nyingine zinasema, kundi la Hamas linaendelea kurusha roketi dhidi ya Israel kwa kutumia vifaa vilivyotengenezwa nchini Iran ambavyo vinaweza kufikisha roketi mpaka Jerusalem na Tel Aviv nchini Israel.