Shirika la habari la AhlulBayt (a.s) ABNA: likinukuu kutoka gazeti la mwananchi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru viongozi saba wa Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) baada ya kuwaona kuwa hawana hatia katika mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili ya njama na matumizi mabaya ya madaraka.
Viongozi hao walioachiwa huru jana na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana ni: Kanali Ayoub Mwakang’ata, Luteni Kanali Mkohi Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajenti John Lazier, Meja Yohana Nyuchi na Mkurugenzi wa Miradi ya Matrekta, Luteni Kanali Felix Samillan. Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Katemana alisema amepitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, vielelezo 25 vya ushahidi walivyoviwasilisha na ushahidi wa upande wa utetezi ulitolewa na washtakiwa, mashahidi wao tisa pamoja na vielelezo vitano na kwamba hakuna ubishi kuwa washtakiwa hao walikuwa wajumbe wa bodi ya Suma JKT pia wakurugenzi wa Bodi ya Takopa na watia saini wa kampuni hiyo walihamisha Sh3.8 bilioni kutoka Takopa kwenda Suma JKT kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa na wanahisa hao kupitia nafasi zao.
“Shtaka hili la matumizi mabaya ya madaraka ni lazima lionyeshe lengo la kujipatia faida au manufaa, si tu kutekeleza sheria, kwa maana hiyo Mahakama hii kwa kulinganisha ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi, unathibitisha mashtaka yao hayawezi kusimama,” alisema Hakimu Katemana.
“Kwa kuwa walitekeleza majukumu yao kama watia saini wa Kampuni ya Takopa licha ya kuwa ni wajumbe wa bodi ya Suma JKT na hakuna kinachoonyesha kuwa walipata manufaa ya aina yoyote ile, hawana hatia na Mahakama imeamua kuwaacha huru watuhumiwa hao
Rejea:mwananchi