Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameyashutumu mataifa ya magharibi kwa kutaka kulazimisha mabadiliko ya utawala nchini Urusi kwa kupitia vikwazo kuhusiana na mzozo wa Ukraine.
Akizungumza katika kikao cha wachambuzi wa kisiasa mjini Moscow leo hii Lavrov amesema mataifa ya magharibi yameonyesha wazi wazi kwamba hayataki kuilazimisha Urusi ibadili sera bali kufanikisha mabadiliko ya utawala nchini humo.Lavrov amekaririwa na shirika la habari la Urusi TASS akisema kwamba hivi sasa viongozi wa serikali katika mataifa ya magharibi wanasema ni muhimu kuweka vikwazo ambavyo vitauangamiza uchumi na kuchochea maandamano ya umma dhidi ya serikali.Vikwazo vilivyoowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi kwa kuuchochea uasi mashariki mwa Ukraine vimelenga sekta ya nishati,ulinzi na fedha na kusababisha kuporomoka vibaya kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo rubble pamoja na kuongezeka kwa gharama za maisha.