Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anakutana na mawaziri wenzake wa Iran na Marekani Mohamed Javad Zarif na John Kerry leo mjini Vienna, kujaribu kuondoa vizingiti vya mwisho katika kufikiwa makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Jamhuri ya kiislamu ya Iran inajadiliana na Uingereza, China, Ufaransa, Urusi , Marekani na Ujerumani kwa lengo la kufikia makubaliano ya kadhia ya nyuklia kabla ya kufika muda wa mwisho wa majadiliano uliowekwa ambao ni Jumatatu ijayo, majadiliano haya yakifanikiwa yata maliza kutengwa kwa Jamhuri ya kiislamu ya Iran kimataifa na kuondolewa kwa vikwazo. Jamhuri ya kiislamu ya Iran kwa upande wake inatakiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa shughuli zake za kinyuklia.Steinmeier amesema kwamba mazungumzo kati ya Iran na madola hayo sita yako wazi na kwamba licha ya tafauti ziliopo pande hizo zimekaribiana zaidi kuliko ilivyokuwa kwa kipindi cha miaka 10 iliopita.Pindi makubaliano hayo yatafikiwa, yatamaliza mgogoro juu ya mpango huo wa nyuklia wa Iran uliodumu kwa miaka 12.
Yafaa kuashiria kwamba Jamhuri ya kiislamu ya Iran bado inashikilia msimamo wake kwamba haina lengo la kutengeneza makombora ya nyuklia.