Rais wa Urusi Vladmir Putin ameitumia hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa, kuzishutumu nchi za magharibi kwa kuutumia mgogoro wa Ukraine ili kuidhoofisha serikali yake.
Putin amesema hakuna atakayefanikiwa katika kuwa na ubabe wa kijeshi kuliko Urusi akiongeza kuwa jeshi lake ni la kisasa, tayari kwa vita, pampja na kuwa ni tulivu kama wasemavyo watu. Putin amesema Urusi ina majeshi ya kutosha ambayo yamejitolea kuulinda uhuru wake. Rais huyo wa Urusi ameongeza kuwa jimbo la Crimea ni "takatifu" kwa Urusi. Amesema Urusi ina haki kuchukua msimamo kuhusu suala la Ukraine na kuwa serikali yake haitaharibu mahusiano na nchi za magharibi licha ya kuwepo malumbano kati yake na Umoja wa Ulaya na Marekani. Amepuuzilia mbali masaibu ya nchi hiyo wakati uchumi ukiendelea kuporomoka kutokana na vikwazo vya nchi za magharibi pamoja na kupungua bei za mafuta.