Raia wa Tanganyika leo hii wanasherekea miaka hamsini na tatu tangu nchi hiyo yenye utajiri mkubwa kupata uhuru kutoka mikononi mwa waingereza.
Tanganyika ni jina la kihistoria la sehemu kubwa ya Tanzania isiyo chini ya serikali ya Zanzibar. Mara nyingi huitwa "Tanzania bara" ingawa kuna visiwa pia, hasa Mafia na Kilwa.
Tanganyika ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki. Imepakana na Uganda na Kenya upande wa Kaskazini, Zanzibar na Bahari Hindi upande wa mashariki, Msumbiji, Malawi na Zambia upande wa kusini, Kongo, Burundi na Rwanda upande wa magharibi.
Tanganyika iliwahi kuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia halafu ikawa chini ya Uingereza kama eneo la kudhaminiwakutokana na azimio la Shirikisho la Mataifa iliyoweka Tanganyika katika ngazi "B" ya maeneo ya kudhaminiwa.
Tanganyika na Zanzibar zilikuwa nchi mbili tofauti hadi 1964, zilipoungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapo kiongozi wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kuwa Rais wa kwanza na kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar Abedi Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Tanganyika ilikuwa koloni ya Uingereza kuanzia 1919 na nchi huru kati ya 1961 hadi 1964. 1964 iliungana na Zanzibar na kuwa sehemu ya Jamhuri ya Maungano ya Tanzania.
Tanzania imekuwa ni nchi ya kupigiwa mfano katika dunia kwani ni nchi iliyoweza kudumisha amani na pia imeweza kukuza lugha yake ya asili ya kiswahili ambayo kwa sasa ndio utambulisho mkuu wa taifa hilo, kwani lugha hii inayafanya makabila 120 ya Tanzania kuweza kuwasiliana bila wasiwasi. Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
