1 Januari 2015 - 19:31
Afghanistan yaadhimisha kuchukua madaraka ya ulinzi

Majeshi ya usalama ya taifa nchini Afghanistan yamechukua madaraka kamili ya usalama nchini humo leo,

Majeshi ya  usalama ya  taifa nchini  Afghanistan  yamechukua madaraka  kamili  ya  usalama  nchini  humo leo, wakati  majeshi  ya NATO  yanayoongozwa  na  Marekani  yakimaliza  ujumbe  wao  wa miaka  13  wa mapambano  na  kuanza  awamu  mpya  ya  kutoa mafunzo, ushauri  na  msaada.

Rais Ashraf Ghani  wa  Afghanistan  akiadhimisha  hatua  hiyo  ya mabadiliko, amesema  anawapongeza  Waafghanistan  katika  siku hii  ya  kihistoria. Ameongeza  kuwa  nchi  hiyo  haitaruhusu  ardhi yake  kutumiwa  dhidi  ya  majirani  zake na  anatarajia  hatua  kama hiyo  itachukuliwa  na  majirani  wa  nchi  hiyo.

Ghani  amesema   majeshi  ya  Afghanistan hivi  sasa  yanawajibika kikamilifu kwa  usalama  wa  nchi  yote, wakati  ikihangaika kupambana  na  wapiganaji. Marekani  na  mataifa  mengine  ya magharibi  imesema  walianzisha  ujumbe  wa  kijeshi  ambao umeiondoa  madarakani  serikali  ya  Taliban  mwaka  2001 kuizuwia Afghanistan  kuwaficha  magaidi  ambao  huenda  wangefanya mashambulizi  nje  ya  nchi hiyo, kufuatia  mashambulizi  ya  kujitoa muhanga  ya  Septemba  11 nchini  Marekani.