Korti moja katika mji mkuu wa Misri, Cairo imewahukumu adhabu ya kifo watu 183, kuhusiana na mashambulizi yaliyofanywa kwenye kituo cha polisi na kuwauwa maafisa 15 baada ya kuangushwa kwa serikali ya rais Mohammed Mursi mwaka 2013.
Hukumu hiyo ni miongoni mwa nyingine kadhaa za vifo dhidi ya watu wengi, ambazo zimezusha lawama za watetezi wa haki za binadamu nchini Misri kwenyewe na katika jumuiya ya kimataifa. Hukumu ya leo imetolewa na Jaji Mohammed Nagi Shehata, ambaye amepata umaarufu katika kutoa huku kali kwa watu wanaodhaniwa kuwa wapinzani wa serikali.
Jaji Shehata aliwahukumu wanaharakati maarufu wa mageuzi kwenda jela kwa kukiuka sheria mpya inayokataza maandamano yasio na kibali, na pia waandishi wa kituo cha televisheni cha Al Jazeera, akiwemo Peter Greste ambaye ameachiwa huru leo.
Wakati hayo yanaendelea rais wa Misri Abdulfatah Sisi ameapa kupambana na magaidi na kusema kwamba Jeshi lake halitatulia mpaka lilipe kikasi nakuwaangamiza magaidi wanao hatarisha amani ya Misri.