Rais Barack Obama na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wameelezea juhudi za pamoja za kufikiwa suluhisho la muda mrefu la kidiplomasia katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine hapo jana.
Rais Barack Obama na kansela wa Ujerumani Angela Merkel jana katika Viongozi hao hata hivyo hawajatoa njia ya wazi ya vipi mataifa ya magharibi yataweza kusonga mbele iwapo mazungumzo ya kuleta amani wiki hii yatakwama.
Obama ameonesha uwezekano kwamba Marekani inaweza kwa mara ya kwanza kutuma silaha za kupambana na vifaru pamoja na silaha nyingine za kujihami nchini Ukraine. Wakati hakuna uamuzi ambao umekwisha chukuliwa, rais Obama amesema ameamuru kikosi chake kutafakari "Iwapo kuna vitu vingine vya ziada vinavyoweza kufanywa kuisaidia Ukraine kuimarisha ulinzi wake katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Urusi.
"Kile nilichokiagiza kikosi changu ni kuangalia hatua mbali mbali za kuchukua. Ni njia gani nyingine zinaweza kuchukuliwa kumfanya Bwana Putin abadilike na uwezekano wa silaha kali za ulinzi ni moja katika nafasi hizo ambazo zinachunguzwa."
Suluhisho la kijeshi
Lakini kansela wa Ujerumani Angela Merkel anapinga vikali kulipatia silaha jeshi la Ukraine lililozingirwa. Kansela wa Ujerumani, ambaye huenda ana uhusiano mzuri zaidi na rais wa Urusi Vladimir Putin , ameweka wazi kwamba hajakata tamaa juu ya uwezekano wa majadiliano ya kidiplomasia kuweza kuleta mpango wa amani ambao hadi sasa haujapatikana.
"Kila mara imethibitika kuwa ni sahihi kujaribu tena na tena kutatua mzozo kama huu," Merkel amesema.
"Sioni kabisa uwezekano wa suluhisho la kijeshi, lakini tunapaswa kufanyakazi kutafuta zaidi suluhisho la kidiploamsia."
Baadaye jana katika mkutano na waandishi habari pamoja na waziri mkuu wa Canada Stephen Harper, Merkel amesisitiza , "Nina matumaini kwamba tutaweza kutatua mzozo huu kwa njia za kidiplomasia kwasababu nafikiri kwa njia za kijeshi mzozo huu hauwezi kutatuliwa."
Harper amesema anafurahia juhudi za Ujerumani na Ufaransa kuleta suluhisho la amani lakini ameongeza: "Kwa bahati mbaya katika wakati huu Bwana Putin amekataa njia za kidiploamasia. Anaonekana kuelekeza ajenda zake kupitia matumizi ya nguvu.
Wakati huo huo zaidi ya wanajeshi 600 wa Urusi wameanza luteka ya kijeshi katika jimbo la Crimea, leo siku moja kabla ya mkutano kuhusu mzozo wa Ukraine katika mji mkuu wa Belarus Minsk.
Seneta John McCain amekaririwa akisema katika Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba "Waukraine wamekuwa wakiuwawa na wao wamekuwa wakiwapelekea mablanketi ambayo hayasaidii kitu kukabiliana na vifaru vya Urusi."
Lakini Merkel ametamka wazi msimamo wake wa kuipatia silaha serikali ya Ukraine kwa kusema kwamba "anafahamu mjadala huo lakini anaamini kutolewa kwa silaha zaidi hakutopelekea kupatikana kwa maendeleo inayoyahitaji Ukraine na kwamba anatilia shaka sana jambo hilo."
Merkel ambaye anazungumza lugha ya Kirusi na ambaye amekulia Ujerumani ya mashariki amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhisho la kidiplomasia ambapo amezungumza na Putin mara kadhaa katika kipindi cha mwaka mmoja na kukutana naye nchini Urusi, Australia na Italia katika miezi ya hivi karibuni.
Serikali ya Urusi imeonya leo hii kwamba Putin hawezi kuzungumziwa katika lugha ya vitisho vya kumuwekea muda wa mwisho kutekeleza maagizo. Alipoulizwa juu ya tetesi za vyombo vya habari kwamba Merkel alimpa muda mwisho Putin katika mazungumzo ya kutayarisha mkutano wa kilele wa Minsk, msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov ameiambia radio ya Govorit Moskva kwamba "hakuna mtu aliyewahi katu kuzungumza na rais huyo kwa lugha ya kumpa muda wa mwisho na hawawezi kufanya hivyo hata kama wangelitaka iwe hivyo."
Obama inabidi aamuwe iwapo atume silaha kwa Ukraine,iweke vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi kwa matarajio ya kumlazimisha Putin akubali kufikia muafaka au aunge mkono kikamilifu juhudi mpya za kutafuta amani za Ujerumani na Ufaransa.
Maafisa wa serikali ya Marekani wanasema atatafakari maamuzi yake kwa uangalifu na hatofanya pupa katika kutowa uamuzi.
Tayari kiongozi huyo ana mapendekezo mezani mwake juu ya hasara na manufaa ya kuipatia Ukraine silaha kama zile za kupambana na vifaru,silaha ndogo ndogo na risasi.
Baadhi ya washauri wake wakuu akiwemo yule aliyemteuwa kuwa waziri mpya wa ulinzi Ashton Carter wanapendelea kusaidiwa kijeshi kwa Ukraine.
Nayo majeshi ya serikali ya Ukraine yanaripotiwa kupata mafanikio katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi mashariki mwa Ukraine.
Msemaji wa jeshi la Ukraine Eduard Basurin amesema jana tarehe 9 mwezi wa 2 mwaka 2015 kuwa wameuzingira mji wa Debaltseve , ambao umekuwa ukikabiliwa na mapigano makali katika muda wa wiki zilizopita, na kuutenga mji huo na barabara kuu.