26 Februari 2015 - 10:05
 Marekani yaionya Urusi kwa vikwazo zaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ameikosoa vikali Urusi kwa kutoheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano ya Minsk, akirejelea onyo la vikwazo zaidi dhidi ya nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ameikosoa vikali Urusi kwa kutoheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano ya Minsk, akirejelea onyo la vikwazo zaidi dhidi ya nchi hiyo. Akizungumza mbele ya wabunge mjini Washington hapo jana, Kerry alisema kufikia sasa si Urusi wala vikosi inavyoviunga mkono mashariki mwa Ukraine, ambavyo vimeheshimu ahadi zao. Juzi Kerry alisema kuwa serikali ya Urusi imekuwa ikimdanganya hata yeye binafsi juu ya kile kinachoendelea mashariki wa Ukraine. Urusi inakanusha madai ya mataifa ya Magharibi kwamba inawaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine. Wakati huo huo, Urusi imetishia kuikatia Ukraine huduma ya gesi, endapo serikali mjini Kiev itashindwa kulipa limbikizo lake la madeni. Ikiwa hatua hiyo itachukuliwa, itayaathiri mataifa kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Wakati hayo yanajiri Umoja wa Ulaya umetangaza mipango ya kuifanyia marekebisho sekta yake ya nishati, kwa lengo la kukabiliana na utegemezi wake kwa Urusi. Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ulaya anayehusika na nishati, Maros Sefcovic, alisema hapo jana kwamba Umoja huo utapitia kwenye kipindi kizito cha mpito kwenye nishati, akiuita mpango huo kuwa ni mkubwa kabisa kuwahi kutekelezwa tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Makaa ya Mawe na Chuma barani Ulaya, zaidi ya miaka 50 iliyopita, na ambayo ndio chanzo cha Umoja wa sasa wa Ulaya. Ulaya inaitegemea Urusi kwa asilimia 40 ya gesi inayotumia. Kwa mujibu wa maelezo ya mpango huo, kutajengwa miundombinu itakayoziruhusu nchi wanachama kupeana huduma ya gesi, kukomesha usimamizi wa bei, kuongeza vinu vya gesi iliyo kwenye mfumo wa kimiminika, na kuimarisha upatikanaji taarifa kati ya kampuni na mataifa wanachama juu ya mapatano na wazalishaji wakubwa wa gesi, kama vile Urusi.