Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Pavlo Klimkin ameonesha wasi wasi wake leo kuhusiana na matarajio kwamba makubaliano yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya kusitisha mapigano na waasi wanaoiunga mkono Urusi yataendelea, wakati akitoa wito wa kupanuliwa kwa kikosi cha kimataifa cha kuangalia makubaliano hayo.
Klimkin amewaambia waandishi habari mjini Tokyo kwamba hali katika eneo la mapigano ni mbaya na ya wasi wasi licha ya makubaliano hayo. Amesema bado kuna makombora kadhaa yanavurumishwa na magaidi mashariki mwa Ukraine.
Klimkin ambaye yuko Japan kwa mkutano na waziri mkuu Shinzo Abe pamoja na mwenzake wa Japan Fumio Kishida amesema hayo siku moja baada ya mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na wa Urusi Sergei Lavrov wameeleza matumaini ya tahadhari kufuatia mazungumzo yao mjini Geneva jana.
Wakati huo huo duru katika jeshi la Ukraine zimesema leo wanajeshi watatu wa Ukraine wameuwawa na wengine tisa wamejeruhiwa katika muda wa masaa 24 yaliyopita katika mapigano na waasi mashariki mwa nchi hiyo.