Magaidi wa kundi la Daesh linalojiita Dola la Kiislamu wamechoma moto visima vya mafuta kwenye mji wa Tikrit ili kuzuia operesheni dhidi yao inayoendeshwa na ndege za kijeshi za Iraq. Magaidi wa kundi la Daesh waliteka visima vingi vya mafuta, na wamekuwa wakichukua mafuta na kuyauza nchi za jiran. Tangu Jumatatu hii, jeshi la Iraq limefanya operesheni kubwa kuliko zote zilizowahi kuendeshwa dhidi ya Magaidi wa kundi la Daesh katika mjini humo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu wapatao 28,000 wameukimbia mji huo ambao ni nyumbani kwa rais wa zamani wa Iraq, Dikteta Saddam Hussein. Iwapo askari watafanikiwa kuikomboa Tikrit basi itakuwa rahisi zaidi kwao kuelekea kaskazini mwa nchi na kupigana na waasi mjini Mosul.
Mipango na ramani ya mashambulizi yanayofanya na jeshi la Iraq, zimepangwa na mtaalamu wa vita wa Iran, viongozi wa jeshi la Marekani wamesema kuwa mpango huo ni wa hali ya juu na wanahakika utafanikiwa.
Na huko Syria watu wasiopungua 34 wameuawa katika mji wa Aleppo baada ya magaidi wa Al nusra kuvamia makao makuu ya shirika la ujasusi. Kwa mujibu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu Syria lenye makao yake makuu London, waasi walikuwa wamechimba njia chini ya jengo hilo na kisha wakalipua bomu ambalo lilisababisha sehemu ya jengo kubomoka. Kundi la kigaidi la al-Nusra lenye mafungamano na al-Qaeda limekiri kufanya mashambulizi hayo ambayo ni mazito zaidi kutokea tangu Jumapili ambapo magaidi hao walikataa pendekezo la kusitisha mapigano katika mji wa Aleppo uliopo Kaskazini mwa Syria. Mapigano katika mji huo ambao ulikuwa mji muhimu kibiashara, yamekuwa yakiendelea tangu mwaka 2012. Magaidi wa al-Nusra wanapata msaada kutoka kwa Israel na Jordan ili kuiangusha serikali ya Syria, lakini magaidi hao pamoja na kupata misaada na vifaa vya kisasa vya kivita wameshindwa kusonga mbele kutokana na udhibiti na ustadi wa hali ya juu wa majeshi ya Syria yakishirikiana na Hizbullah.