6 Machi 2015 - 19:41
Umoja wa Mataifa walaani kubomolewa turathi za Iraq

Umoja wa Mataifa umelaani vikali kampeni inayoendeshwa na kundi la kigaidi la Daesh ya kuvunja na kuharibu turathi za kihistoria katika miji kadhaa wanayoidhibiti nchini Iraq.

Umoja wa Mataifa umelaani vikali kampeni inayoendeshwa na kundi la kigaidi la Daesh ya kuvunja na kuharibu turathi za kihistoria katika miji kadhaa wanayoidhibiti nchini Iraq.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Paris hivi leo, mkuu wa shirika linaloshughulikia utamaduni kwenye Umoja wa Mataifa alisema kitendo kilichofanywa na kigaidi la Daesh kwenye makumbusho moja huko Iraq ni sawa na "maangamizi dhidi ya utamaduni"

"Ni maangamizi dhidi ya utamaduni. Hakuna neno jengine la kuelezea kile kinachotokezea. Ni maangamizi ya wazi dhidi ya utamaduni. Kwa kusema ukweli, sikuweza kuziangalia picha za maangamizi hayo hadi hapo jana. Zilikuwa zinatisha. Zinaogofya hasa. Sikuweza kuziangalia mpaka mwisho." Alisema Irina Bokova, mkurugenzi mkuu wa UNESCO, akisisitza kuwa vitendo hivyo ni sawa na uhalifu wa kivita na akitoa wito kwa dunia iwaadhibu wale walioutenda.

Msimamo huu wa UNESCO ulikuja siku moja tu baada ya vidio kusambazwa mitandaoni ikiwaonesha wanamgambo wa kigaidi la Daesh wakiharibu vitu vya kale vya zama za Mesopotomia katika makumbusho moja mjini Mosul, mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq.

Jengo la kale Nimrud laangushwa

Taarifa kutoka mji wa kale wa zama za Assyria wa Nimrud zinasema wanamgambo hao waliliangusha jengo jengine lenye umri wa miaka 3,000 kwenye Mto Tigris. Mji wa Nimrud ulio umbali wa kimolita 30 kusini mwa Mosul, ulijengwa miaka 1250 kabla ya kuzaliwa Kristo.

Ni mji huo ambao karne nne baadaye ulikuja ukawa makao makuu ya dola ya Assyria, ambalo kwa wakati huo ndilo lililokuwa dola lenye nguvu kabisa duniani, likitawala kutokea Misri ya leo, hadi Uturuki na Iran.

Ubomoaji huo ulikuwa ni sehemu ya kampeni ya kundi hilo la siasa kali ambalo hadi sasa limeshaharibu maeneo kadhaa matukufu na ya kihistoria, zikiwemo nyumba za ibada za Waislamu, katika kile wanachosema ni kuteketeza Bidaa (uzushi) kwenye Uislamu, kama  ilivyo itikadi ya waislamu wa dhehebu la Sunni la Wahabia

Iraq yaomba silaha zaidi kunusuru turathi zake

Balozi wa Iraq kwenye shirika hilo la UNESCO, Mahmoud Khalaf, amelitolea wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuipa nchi yake msaada wa kijeshi ili kuwazuia wanamgambo wa kigaidi la Daesh wasiendelee na uharibifu wao wa turathi za kilimwengu zilizoko Iraq.

Tunadhani kukanusha na kulaani tu hakutoshi. Tunalitaka Baraza la Usalama na nchi zote duniani kushirikiana na Iraq, kutusaidia kwa silaha. Madhali Mosul au sehemu nyengine yoyote ya Iraq imekaliwa na kundi hili la uharibifu, uhalifu utaendelea na alama na turathi za Iraq zitateketezwa zote," alisema Khalaf akiwa mjini Paris kushiriki kikao na wakuu wa UNESCO.