Venezuela imesema imemuita balozi wake mjini Washington Maximilien Sanchez arejee nyumbani baada ya vikwazo vya Marekani dhidi ya maafisa wake. Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ameikosoa vikali Marekani kwa kuwawekea vikwazo maafisa wa Venezuela wanaoshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu, akisema ataliomba bunge limpe mamlaka zaidi kupambana na kitisho cha ubeberu.
Marekani imeitangaza Venezuela kuwa kitisho kwa usalama wa taifa na kuamuru vikwazo dhidi ya maafisa saba katika mzozo mbaya kabisa wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, tangu rais Maduro alipoingia madarakani mnamo mwaka 2013. Hapo jana rais wa Marekani Barack Obama alisaini na kutoa amri ya kiutendaji ambayo haikuilenga sekta ya nishati ya Venezuela wala uchumi wake, lakini inayoongeza wasiwasi kati ya nchi hizo mbili, huku Marekani ikifanya juhudi za kurejesha uhusiano wa kawaida na Cuba, mshirika wa karibu wa Venezuela huko Amerika Kusini.