12 Machi 2015 - 14:40
 Mgombea umeya akutwa amekatwa kichwa Mexico

Mgombea wa nafasi ya meya kutoka vyama vya mrengo wa shoto nchini Mexico amekutwa akiwa ameuawa na kukatwa viungo. Aide Nava anaaminika kuwa alitekwa na genge la wahalifu hapo Jumatatu.

 

Mgombea wa nafasi ya meya kutoka vyama vya mrengo wa shoto nchini Mexico amekutwa akiwa ameuawa na kukatwa viungo. Aide Nava anaaminika kuwa alitekwa na genge la wahalifu hapo Jumatatu. Mamlaka za jimbo la Guerrero zinasema mwili wa mgombea huyo ulipatikana hapo juzi. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya huko, genge la kihalifu liitwalo Los Rojos limewatishia wanasiasa wengine kupatwa na yaliyomsibu Aide Nava, aliyekuwa na miaka 42. Mwaka jana, wahalifu wa madawa ya kulevya walimuua mume wa Nava, ambaye ndiye aliyekuwa meya. Mtoto wao wa kiume aliyetekwa mwaka jana, bado hajaonekana mpaka sasa. Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Guerrero, Miguel Angel Godinez, alisema hapo jana kwamba hali imekuwa ngumu sana na tahadhari ya hali ya juu inahitajika. Ndani ya kipindi cha miaka minane iliyopita, zaidi ya watu 100,000 wameshauawa na makundi yanayofanya biashara haramu ya madawa ya kulevya.