21 Machi 2015 - 19:24
Yemen ipo katika hatari ya kugawanyika

Rais wa Yemen anayekabiliwa na mzozo amesema mauaji ya kujitowa muhanga yaliouwa watu 142 katika misikiti ya wanamapinduzi wa kishia wa huthi yamekusudia kuitumbukiza nchi kwenye machafuko,umwagaji damu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Rais wa Yemen anayekabiliwa na mzozo amesema mauaji ya kujitowa muhanga yaliouwa watu 142 katika misikiti ya wanamapinduzi wa kishia wa huthi yamekusudia kuitumbukiza nchi kwenye machafuko,umwagaji damu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Abedrabbo Mansour Hadi aliyekimbia kutoka kifungo cha nyumbani katika mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na wanamapinduzi wa kishia wa Huthi na kujihifadhi katika mji wa Aden ulioko kusini mwa nchi hiyo mwezi uliopita,amelaani mashambulizi hayo kuwa ni ya kigaidi,uhalifu na woga.

Katika baruwa kwa familia za wahanga na watu waliojeruhiwa 351 iliyotolewa na ofisi ya rais huyo Ijumaa usiku imesema mashambulizi hayo ya kinyama yanaweza tu kufanywa na maadui wa uhai ambao wanataka kuitumbukiza Yemen kwenye machafuko, umwagaji damu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Hadi ameandika katika baruwa hiyo kwamba Mashia wa itikadi kali wanaowakilishwa na wanamgambo ambao ni  wanamapinduzi wa kishia wa Huthi na Wasunni wa itikadi kali wanaowakilishwa na kundi la kigaidi la Al-Qaeda ni sehemu mbili zilioko kwenye sarafu moja ambazo haziitakii mema na utengamano Yemen na watu wake.

Miripuko ya maafa

Miripuko kadhaa ya mabomu ya kujitowa muhanga yaliodaiwa kufanywa na kundi la kigaidi la Daesh imeuwa takriban watu 142 hapo Ijumaa katika misikiti ya wanamapinduzi wa kishia wa Huthi katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa ikiwa ni mojawapo ya mashambulizi ya maafa makubwa kuwahi kufanywa na magaidi hao wa kundi la Daesh linalopata udhamini toka Saudia arabia.

Mashambulizi hayo ni ya kwanza kudaiwa kufanywa na kundi la la kigaidi la Daesh nchini Yemen na yanaonyesha nguvu kubwa iliokuwa nayo kundi hilo katika nchi ambayo kundi hasimu la Al Qaeda ndio mashuhuri kabisa miongoni mwa makundi wa wapiganaji wa kigaidi, kundi la Al Qaeda limekanusha kuhusika na mauaji hayo kwa kusema kwamba mikakati yake sio kushambulia misikiti.

Waumini waliwakimbiza hospitali majeruhi kwa kutumia malori wakati watu wengine wakiondowa miili iliyokatika vipande vipande.Mshambuliaji mmoja wa kujitowa muhanga aliulenga msikiti wa Badr kusini mwa Sanaa wakati mshambuliaji mwengine aliwashambulia waumini waliokuwa wakikimbia nje kutoka msikiti huo.

Mshambuliaji wa tatu aliulenga msikiti wa Al-Hashush kaskzini mwa Sanaa wakati mshambuliaji wa nne alijiripuwa nje ya msikiti huo ambao hivi sasa unadhibitiwa na wanamapinduzi wa kishia wa Huthi.Imam wa msikiti wa Badr alikuwa miongoni mwa watu waliouwawa. Duru zinasema mshambuliaji mwengine alijiripua nje ya msikiti katika ngome kuu ya wanamapinduzi wa kishia wa Huthi ilioko katika mji wa Saada kaskazini mwa Yemen baada ya kushindwa kuingia ndani ya msikiti kutokana na usalama mkali. Mshambuliaji huyo alikuwa ni mtu pekee aliyepoteza maisha yake.

Mashambulizi ni mwanzo tu

Kwa mujibu wa Televisheni ya wanamapinduzi wa kishia wa Huthi  hospitali zilikuwa zinatowa wito kwa watu kuchangia damu.Katika taarifa iliyotolewa kwenye mtandao tawi la kundi la kigaidi la Daesh mjini Sanaa limesema mashambulizi hayo ni "mwanzo tu".

Kundi la kigaidi la Daesh limesema “Makafiri wa Kihuthi wanapaswa kujuwa kwamba wanajeshi wa Daesh hawatopumuwa hadi hapo watakapowatokomeza wahuthi na kuukata mkono wa Iran kwa mpango wake ilio nao kwa Yemen”.

Wanamapinduzi wa kishia wa Huthi wanatuhumiwa kupatiwa msaada na Iran, na kundi la kigaidi la Daesh linatuhumiwa kupata msaada wa moja kwa moja kutoka kwa Saudia arabia na Marekani.

Mashambulizi hayo ya Ijumaa yamekuja siku moja baada ya mapambano kati ya vikosi tiifu kwa Rais Hadi na vile vinavyowaunga mkono wanamapinduzi wa kishia wa Huthi katika mji wa kusini wa Aden.

Tokea kukimbilia Aden mwezi uliopita,Hadi amekuwa akihangaika kuimarisha madaraka yake na hapo Alhamisi kiongozi huyo ilibidi aondolewe kwenye kasri la rais mjini Aden baada ya ndege ya kivita kufanya mashambulizi na kuuripua mlima ulioko karibu na kasri hilo.

Katika shambulio jengine tafauti hapo Alhamisi watu 11 waliuwawa wakati wapiganaji wa vikosi maalum tiifu kwa wanamapinduzi wa kishia wa Huthi walipojaribu kuuteka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden kutoka kwa wanamgambo walio tiifu kwa Hadi mapigano ambayo yalipelekea kufungwa kwa uwanja wa ndege huo.Hata hivyo uwanja wa ndege huo umefunguliwa tena Ijumaa.

wanamapinduzi wa kishia wa Huthi wanyatia maeneo ya kusini

Kufuatia wanamapinduzi wa kishia wa Huthi kuuteka mji mkuu wa Sanaa,Saudi Arabia na nchi nyengine za Ghuba zimehamishia ofisi zao za ubalozi mjini Aden na balozi kadhaa za mataifa ya magharibi zimefunga balozi zao katika mji mkuu wa nchi hiyo kwa sababu za usalama.

Tokea wanamapinduzi wa kishia wa Huthi walipoudhibiti mji wa Sanaa hapo mwezi wa Septemba wamekuwa wakizidi kuimarisha hatamu zao madarakani katika vituo vya serikali wakisaidiwa na vikosi vilio tiifu kwa Rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Lakini harakati zao za kutaka kudhibiti maeneo ya kusini zimekuwa zikikabiliwa na upinzani mkali wa vikosi vya kikabila vya madhehebu ya Sunni vyenye mafungamano na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Qaeda ambao bado wana nguvu nchini Yemen.Kutokana wanamapinduzi wa kishia wa Huthi kuendelea kuudhibiti mji mkuu wa Sanaa, Hadi ameutangaza Aden kuwa mji mkuu wa muda nchini Yemen.