Wachunguzi wamepata sauti zilizorekodiwa katika moja kati ya visanduku vyeusi vinavyorekodi taarifa za safari za ndege katika ndege ya shirika la Germanwings ambayo ilianguka katika milima ya Alps , na kuuwa watu wote waliokuwamo katika ndege hiyo.
Wachunguzi hao wanatarajia kupata taarifa za mwanzo katika muda wa siku kadhaa, lakini wamesema kazi kubwa zaidi itahitajika kuweza kutafsiri yaliyomo katika chombo hicho.
Jana kansela wa Ujerumani Angela Merkel alijiunga na rais wa Ufaransa Francois Hollande na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy katika milima ya Alps nchini Ufaransa karibu na mahali palipoangukia ndege hiyo, kukutana na wafanyakazi wa uokozi pamoja na wale wa kujitolea.
Wakati huo huo shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa limesema haliwezi kuthibitisha ripoti ya chombo cha habari nchini Marekani juu ya mazingira ambayo yamesababisha kuanguka kwa ndege ya shirika lake tanzu la Germanwings.
Hata hivyo taarifa zinasema mwili wa kwanza wa wahanga wa ajali hiyo umepatikana hii leo.
Gazeti la New York Times limeripoti kuwa sauti zinazosikika kutoka katika eneo la kuendeshea ndege zilizonakiliwa na kisanduku cha kurekodi sauti za marubani katika ndege iliyoanguka ya shirika la Germanwings zinaonesha kwamba rubani mmoja alitoka kutoka eneo hilo na hakuweza kuingia tena kabla ya ndege hiyo kuanguka.
Sauti hiyo iliyorekodiwa haikutoa ishara ni kwanini rubani aliondoka katika eneo hilo na kwanini hakuweza kurejea wakati ndege hiyo ikielekea taratibu milimani siku ya Jumanne.
Mchunguzi katika ajali hiyo ambaye hakutajwa jina amesema mtu aliyekuwa nje ya eneo la kuendeshea ndege alisikika akigonga mlango na hakukuwa na jibu.
Wakati huo huo shirika la ndege la Lufthansa limetayarisha safari kutoka Uhispania na Ujerumani kuwapeleka ndugu wa wahanga wa ajali hiyo katika eneo hilo la milima ya Alps.