Saudi Arabia imeamua kumrejesha balozi wake nchini Sweden, hatua ambayo itapunguza mgogoro wa kidiplomasia uliyosababishwa na ukosoaji wa rekodi ya haki za binaadamu ya taifa hilo la Kiarabu. Hii ni kwa mujibu wa Televisheni ya Al-Arabiya ya nchini humo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Sweden haikuweza kuthibitisha habari hizo, lakini mwanadiplomasia wa Sweden nchini Saudi Arabia, alimhakikishia Mfalme Salman jana Ijumaa kuwa matamshi yaliyotolewa na waziri wa mambo ya kigeni Margot Wallstrom hayakuwa na nia ya kuikashifu nchi hiyo na Uislamu.
Mwezi Januari, waziri Wallstrom aliandika kwenye mtandao wake wa twitter kuwa hatua ya kuchapwa viboko mwanablogi wa Saudia Raid Badawi, ni jaribio la kukandamiza uhuru wa kisasa wa kujizeleza. Pia alikosoa sera zinazowaathiri wanawake, kama vile marufuku ya kuendesha magari na kutotoka majumbani mwao bila kusindikizwa na ndugu wa kiume. Mgogoro uliyofuatia ulisababisha Saudi Arabia kumzuwia Wallstrom kuhutubia mkutano wa jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu, na baadaye Sweden ikasitisha makubaliano ya muda mrefu ya ushirikiano w akijeshi na Saudi arabia.