Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameazimia kuyajibu vikali mashambulizi ya waasi wa Somalia wa kundi la Al Shabab ambao waliwaua watu 147 katika chuo kikuu cha Garissa kaskazini mwa Kenya Alhamisi wiki hii. Katika hotuba kwa taifa aliyoitoa hapo jana kutoka Ikulu ya Rais, Kenyatta amesema waasisi wa taifa hilo la Kenya walikufa kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo na atafanya kila njia kulilinda taifa hilo.
Rais huyo wa Kenya amelitoa tamko hilo wakati serikali imetangaza kuwa imewakamata watu watano wanaotuhumiwa kuhusika na shambulizi hilo la Garissa. Washukiwa watatu walikamatwa walipokuwa wanajribu kutorokea Somalia na wawili walikamatwa chuoni humo. Mmoja wa washukiwa hao Rashid Charles Mberesero, ametambuliwa kuwa raia wa Tanzania na mwengine ni mlinzi wa chuo hicho cha Garissa anayesemekana kuwa aliwasaidia magaidi hao. Kundi hilo la Al Shabab limeapa kufanya mashambulizi zaidi nchini Kenya hadi itakapoyaondoa majeshi yake Somalia.