Rais wa Marekani Barack Obama amesema ataendelea kushirikiana na washirika wake katika kuangazia vitendo alivyovitaja vya kusababisha msukosuko vinavyofanywa na Iran katika kanda ya Mashariki ya Kati.
Obama amempigia simu mfalme wa Oman Sultani Qaboos na kumuahidi atashirikiana naye pamoja na washirika wengine wa Marekani katika kanda hiyo. Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili ni sehemu ya kampeni ya Marekani kuwahakikishia washirika wake kuwa makubaliano muhimu yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu zaidi duniani kuhusu mpango wake wa kinyuklia hayamaanishi kuwa Marekani inalegeza msimamo wake kuhusu Iran.
Nchi kadhaa za kanda ya Mashariki ya kati zimekuwa zikiilaumu Iran kwa kuchochea mizozo katika eneo hilo ikiwemo Syria,Yemen, Iraq na Lebanon. Wakati huo huo, Rais Obama amepuuzilia mbali msimamo wa Israel kuwa makubaliano kamili kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani yajikite kwa sharti kuwa Iran iitambue Israel kama taifa.
Kwa upande wa Iran nayo imesema kufikia makubalinao ya nyuklia hakumaanishi kuwa rafiki wa Marekani, na kwamba Jamhuri ya kiislamu ya Iran itaendeleza msimamo wake wa kuwatetea wanaodhulumiwa bila ya kujali anayewadhulumu ni Marekani, Saudia arabia, Israel au yeyote yule.
Iran inashutumiwa kwa kuzisaidia serikali za Iraq na Syria kupambana na magaidi wa Daesh ambapo wanaoshutumu wanasema inaningilia masuala ya ndani ya nchi hizo.
Pia inashutumiwa kwa kuwasaidia wananchi wa Lebanon kupambana na Israel pindi ilipowavamia na kuwashambulia kwa ndege za kivita.
Na sasa nchi za kiarabu ambazo ni wafuasi wa Israel na Marekani zinaishutumu Jamhuri ya kiislamu ya Iran kwa kuwaunga mkono wananchi wa Yemen, ambao wanapigwa vita na muungano wa nchi za kiarabu baada ya kumkataa rais Hadi ambaye wananchi hao, hawamtaki kutokana na kuwa na misimamo ya kufuata upepo wa Saudia arabia, Israel na Marekani.
Wananchi wa Yemen wanasema kuwa Yemen ni nchi huru na wala haihitaji nchi yeyote kuingilia mambo yake ya ndani kama vile ambavyo rais Hadi alivyokuwa akiruhusu nchi za kigeni kuwa na hisa katika uongozi na utawala wa taifa hilo la huru la kiarabu.