Jopo la bunge la Marekani lenye kuchunguza mashambulizi ya mwaka 2012 dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi Libya jana limemtaka waziri wa zamani wa mambo ya nje Hilary Clinton afike kwenye vikao viwili vya hadhara bungeni kutowa ushahidi wake.
Mwenyekiti wa Tume ya Benghazi Trey Gowdy amemuandikia Mwendesha Mashtaka akiomba ushiriki wa Clinton katika vikao hivyo ambacho cha kwanza kitafanyika mwezi ujao katika tarehe itakayotangazwa baadae. Clinton ametangaza ugombea wake katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 na atatarajiwa kujitowa kwa muda kwenye mkondo wa kampeni ili aweze kuhudhuria vikao hivyo katika bunge la Marekani.Kikao cha kwanza kitajikita mahsusi katika matumizi ya anwani binafsi ya baruwa pepe ya Clinton wakati akiwa katika wizara ya mambo ya nje kati ya mwaka 2009 na 2013 jambo ambalo lilikuja kubainika hapo mwezi wa Machi.