10 Juni 2019 - 06:51
Hamas yaitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina ikabiliane na Muamala wa Karne

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inapasa kuunga mkono muqawama mbele ya mpango eti wa amani uliopendekezwa na Marekani kwa jina la "Muamala wa Karne."

(ABNA24.com) Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inapasa kuunga mkono muqawama mbele ya mpango eti wa amani uliopendekezwa na Marekani kwa jina la "Muamala wa Karne."

Hazem Qassem ameyataja matamshi ya David Friedman Balozi wa Marekani katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu kuhusu kuunganishwa sehemu ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuwa yanadhihirisha ni kiasi gani Marekani inashiriki katika kuwakalia kwa mabavu wananchi wa Palestina. Msemaji wa Hamas ameongeza kusema kuwa matamshi ya Friedman yamethibitisha na kuweka wazi fikra za kikoloni za serikali ya Marekani na kufichua ukweli kuhusu Muamala huo wa Karne.

Hazem Qassem amemtaja Balozi huyo wa Marekani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kuwa ni mwakilishi wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na adui wa wananchi wa Palestina. Wakati huo huo makundi ya Palestina yamekosoa matamshi ya Balozi huyo wa Marekani aliyoyatoa huko Baitul Muqaddas kuhusu kuunganishwa sehemu ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kueleza kuwa David Friedman ametoa matamshi hayo ikiwa ni katika kuunga mkono siasa za utawala wa Kizayuni za Kuyahudisha maeneo ya Wapalestina.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la New York Times, Friedman amesema kuwa kuunganishwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni haki ya utawala wa Kizayuni.




/129