26 Juni 2019 - 08:33
Hashdu sh-Sha'abi yafanya operesheni dhidi ya ugaidi katika mkoa wa al-Anbar

Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq, jana ilitekeleza operesheni kali katika ngome za siri za magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS) magharibi mwa mkoa wa Al-Anbar.

(ABNA24.com) Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq, jana ilitekeleza operesheni kali katika ngome za siri za magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS) magharibi mwa mkoa wa Al-Anbar.

Katika operesheni hizo, makumi ya magaidi wa kundi hilo waliangamizwa mkoani hapo. Hii ni katika hali ambayo idara ya intelejensia ya Iraq imetangaza kwamba jeshi la inchi hiyo limefanikiwa pia kuangamiza ngome kadhaa za siri na njia za chini ya ardhi za magaidi hao wa Daesh (ISIS) kusini mwa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa (Nineveh).

Inafaa kuashiria kuwa, licha ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh kushindwa nchini Iraq, lakini hadi sasa bado kuna mabaki ya wanachama wake katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ambao wamekuwa wakitekeleza vitendo vya kigaidi.

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) liliivamia Iraq mwaka 2014 kwa uungaji mkono kamili wa kifedha na kijeshi wa Marekani na washirika wake wa nchi za Magharibi na Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, ambapo liliweza kudhibiti maeneo makubwa ya kaskazini na magharibi mwa Iraq na kutenda jinai kubwa za kutisha dhidi ya wakazi wa maeneo hayo. Kufuatia hali hiyo, Iraq iliiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuisaidia katika kuwaangamiza magaidi hao wakufurishaji.

Tarehe 17 Novemba 2017 jeshi la Iraq na kwa msaada wa washauri wa kijeshi wa Iran, likafanikiwa kutangaza rasmi kushindwa kundi hilo baada ya kudhibiti ngome yake ya mwisho ya Rawa katika mkoa wa Al-Anbar, magharibi mwa nchi hiyo. Kudhibitiwa ngome hiyo, kulifunga rasmi faili la kundi hilo la Kiwahabi nchini Iraq.





/129