1 Julai 2019 - 02:48
Kushindwa ndege ya ujasusi ya Global Hawk, mashitaka ya Iran dhidi ya Marekani

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya sheria na ya kimataifa amesema kuwa, Tehran imeishitaki Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na ndege yake ya ujasusi ya Global Hawk kukiuka anga yake.

(ABNA24.com)  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya sheria na ya kimataifa amesema kuwa, Tehran imeishitaki Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na ndege yake ya ujasusi ya Global Hawk kukiuka anga yake.

Gholam Hossein Dehghani aliyasema hayo Ijumaa akiongea na waandishi wa habari na kubainisha kwamba katika mashitaka hayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha hati ya Umoja wa Mataifa, imesisitiza kuwa iwapo kwa mara nyingine Marekani itakiuka anga yake, basi Iran itakuwa na haki ya kutoa jibu kali kwa ajili ya kujilinda. Itakumbukwa kuwa tarehe 20 mwezi huu ndege ya ujasusi ya Global Hawk ya Marekani na baada ya kukiuka anga ya Iran karibu na Kouh-e-Mobarak katika eneo la Jask mkoani Hormozgan kusini mwa Iran, ilitunguliwa na kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Hatua za Marekani katika maeneo tofauti ya dunia, zinakinzana wazi na sheria za kimataifa. Mienendo hiyo imeshika kasi zaidi baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump. Utumiaji mabavu na kutozingatia sheria na misingi ya kimataifa ni sifa muhimu ya Trump ambayo inatekelezwa katika fremu ya utumiaji mabavu wa moja kwa moja na wa upande katika mfumo wa kimataifa.

Mwenendo huo umehatarisha mfumo unaotawala katika mahusiano ya kimataifa na nchi pamoja na asasi za kimataifa kupuuza mienendo hiyo haribifu ya rais wa Marekani dhidi ya Iran na baadhi ya nchi nyingine, utakuwa na matokeo mabaya zaidi. Hata hivyo isisahulike kuwa, siasa za serikali ya Rais Donald Trump zinakabiliwa na upinzani mkali katika ngazi za kimataifa na hata ndani ya Marekani kwenyewe. Hivyo kadri msimamo imara katika kukabiliana na ubeberu wa upande mmoja wa Trump unavyoongezeka, ndivyo ambavyo usalama na utawala wa pande kadhaa duniani unazidi kudhaminiwa. Kuhusiana na suala hilo Dianne Feinstein, Seneta wa jimbo la California nchini Marekani akizungumza katika bunge la kongresi la nchi hiyo kwamba vita na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si kwa maslahi ya yeyote amesema: "Trump ni lazima ahitimishe siasa na matamshi ya uhasama na badala yake aingie katika uwanja tofauti wa udiplomasia." Aidha Russia na China zikiwa nchi muhimu na zenye nguvu duniani, nazo hazikubali hata kidogo siasa za mabavu za serikali ya Trump duniani, kama ambavyo pia zimeweka wazi upinzani wao kuhusiana na hatua mbovu za Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika uwanja huo, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia hivi karibuni sambamba na kuashiria uamusi wa Marekani wa kuongeza idadi ya askari wake katika eneo la Asia Magharibi alisema: "Russia inasikitishwa sana na kuendelea siasa mbovu za Marekani katika kushadidisha mgogoro na makabiliano na Iran, na pia kuongezwa idadi ya askari wake katika eneo la Asia Magharibi." Kile ambacho kinatekelezwa na serikali ya sasa ya Marekani kwa anwani ya stratijia zake katika eneo la Asia Magharibi, ni uadui na uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuongeza vikwazo vya kiuchumi, vitisho dhidi ya Iran na kushadidisha mzozo katika eneo la Ghuba ya Uajemi, ni ishara za uadui na uhasama huo wa Marekani dhidi ya taifa hili. Hata hivyo msimamo wa Iran si wa kufumbia macho maslahi yake ya kitaifa na ardhi yake na ni kwa ajili hiyo ndio maana kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kikatoa jibu kali kwa kuitungua ndege ya ujasusi ya Marekani iliyokiuka anga yake. Na katika uwanja huo Iran kwa kutegemea sheria na udiplomasia katika kulinda mipaka yake ya anga, bahari na nchi kavu haitosita kuchukua hatua stahiki katika uwanja huo. Kama alivyosema Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo yake ya simu ya  hivi karibuni na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, iwapo Wamarekani watajaribu tena kukiuka maji na anga ya Iran, vikosi vya nchi hii vimepewa amri ya kukabiliana nao vikali.



/129