21 Julai 2019 - 07:56
Zarif akutana na Rais Nicolás Maduro wa Venezuela mjini Caracas

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amekutana na Rais Nicolás Maduro wa Venezuela mjini Caracas.

(ABNA24.com) Katika mazungumzo yao, Zarif na Maduro wamejadili masuala tofauti katika mahusiano ya nchi mbili. Kabla ya hapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikutana na Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez na kufanya naye mazungumzo muhimu. Zarif aliwasili mjini Caracas akitokea mjini New York, Marekani kwa ajili ya kushirikia kikao cha Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).

Katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea wimbi la matukio ya upande mmoja wenye kufurutu ada wa Marekani kuwa ndio changamoto muhimu ambayo inawakabili wote. Ameongeza kwamba kitendo cha kudhoofisha kwa mbinu tofauti mfumo wa utawala wa sheria katika ngazi ya kimataifa, kinatishia kuvuruga amani na uthabiti wa dunia. Aidha kando na mkutano huo, amekutana na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi tofauti. Baada ya kutoka nchini Venezuela, Mohammad Javad Zarif ataelekea nchini Nicaragua na Bolivia zilizo Amerika ya Kusini.



/129