20 Oktoba 2019 - 09:35
Matembezi makubwa ya "Waliosalia Nyuma" katika Arubaini ya Imam Hussein (as) yafanyika mjini Tehran

Matembezi ya "Waliosalia Nyuma" katika Arubaini ya Imam Hussein (as) yamefanyika katika mwendo wa kilomita 17 kuanzia kwenye medani ya Imam Hussein (as) hapa mjini Tehran kuelekea haram ya mtukufu Abdul-Adhim (as) iliyoko mjini Rey kusini mwa Tehran kwa kuhudhuriwa na wapenzi na maashiki wa Imam Hussein (as).

(ABNA24.com) Matembezi hayo ya "Waliosalia Nyuma" katika Arubaini ya Imam Hussein (as) yameanza leo asubuhi kuanzia kwenye medani ya Imam Hussein kuelekea haram ya mtukufu Abdul-Adhim (as).

Naibu wa Meya wa jiji la Tehran, Mojtaba Yazdani amesema, askari wapatao 450 na magari yapatayo 205 yamesindikiza matembezi hayo kwa ajili ya kutoa huduma kwa waumini.

Sambamba na kukaribia kufanyika matembezi makubwa ya "Waliosalia Nyuma" katika Arubaini, asubuhi ya jana, ilifanyika shughuli ya kuinadhifisha na kuinukisha kwa manukato haram toharifu ya mtukufu Abdul-Adhim al-Hassani (as) iliyopo mjini Rey kwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wafuasi na maashiki wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW.

Tangu siku chache nyuma kabla ya kuwadia Arubaini ya Imam Hussein (as) ambaye ni Imam wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, umati mkubwa wa Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo umekuwa ukitembea kwa miguu masafa ya karibu kilomita 80 kutoka mji wa Najaf hadi Karbala nchini Iraq ili kwenda kuzuru Haram toharifu ya mtukufu huyo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na duru za Iraq, mazuwari wanaokadiriwa kufikia milioni 14 walishiriki Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) ya mwaka uliopita, ambao ni mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini unaofanyika kila mwaka duniani.

........
340