(ABNA24.com) Rais Bashar al-Assad wa Syria ameionya Uturuki na kuikosoa Marekani na kuzungumzia uwezekano wa Washington wa kuliunda tena kundi la kigaidi la Daesh na akasisitiza juu ya kulindwa ardhi yote ya nchi hiyo.
Rais Assad amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na vyombo vya habari vya Syria. Tarehe 17 ya mwezi uliopita wa Oktoba, Uturuki ikipata baraka za Marekani ilianza kufanya mashambulio kaskazini mwa Syria mashambulio ambayo yalidumu kwa muda wa wiki moja. Rais Bashar al-Assad amezungumzia mashambulio hayo na kuashiria nukta tatu muhimu.
Nukta ya kwanza ni kuwa, Rais Assad hajayatambua mashambulio hayo ya Uturuki kwamba, nia yake ni kupambana na ugaidi, bali amesema chimbuko lake ni tamaa ya Ankara kwa ardhi ya Syria.
Nukta ya pili ni kwamba, Rais Assad ameitaja Uturuki kama mwakilishi wa Marekani katika eneo. Kwa maneno mengine ni kuwa, Rais Assad anaamini kuwa, Marekani ndiyo iliyotoa idhini ya mashambulio ya Uturuki dhidi ya Syria na hatua hii inapaswa kuwa ibra na funzo kwa baadhi ya makundi ya Syria wakiwemo Wakurdi kwamba, wasitegemee himaya na uungaji mkono wa Washington.
Nukta ya tatu ni kuwa, Rais Bashar al-Assad ameionya Uturuki akiiambia kwamba: Kama haitaondoka katika ardhi ya Syria, basi hakuna chaguo jingine ghairi ya vita. Rais Assad siyo tu kwamba, amesisitiza kuondoka vikosi vya Uturuki katika ardhi ya Syria bali ameyaonya makundi ya wabeba silaha yanayoungwa mkono na serikali ya Ankara katika mkoa wa Idlib kwamba, kama hayataondoka katika ardhi ya Syria na kuelekea Uturuki, basi yanapaswa kuachana na upinzani dhidi ya serikali ya Damascus au yatakabiliwa na operesheni ya jeshi la nchi hiyo ya kuyafurusha katika ardhi ya Syria.
Msimamo huu waRais Bashar al-Assad unaonyesha kuwa, serikali ya Syria imevuka kipindi cha mgogoro na filihali ipo katika mazingira na nafasi nzuri ya kujilinda na kujitetea sambamba na kulinda ardhi yote ya nchi hiyo ni jambo linalopewa kipaumbele na serikali ya nchi hiyo.
Sehemu nyingine ya matamshi ya Rais Bashar al-Assad ilihusiana na siasa za Marekani mkabala na Syria. Kupitia matamshi hayo ya Rais Assad tunaweza kuashiria nukta nne kuu.
Mosi, kwa mtazamo wa Rais Assad ni kuwa, operesheni dhidi ya Abu Bakr al-Baghdadi pamoja na kuuawa kwake, ni hadaa na uongo mtupu, kwani Marekani kwa kumuua kiongozi huyo wa Daesh imefanya juhudi za kurejesha heshima na hadhi yake iliyopotea katika suala zima la kupambana na ugaidi.
Pili, maslahi ya Marekani yapo katika kuanzishwa makundi kama Daesh. Mintarafu hiyo, Rais wa Syria anaamini kuwa, kuna uwezekano wa kuanzishwa tena kundi la Daesh na kuzungumziwa akina Abu Bakr al-Baghdadi wengine. Nukta ya tatu ni kuwa, madai ya Marekani juu ya kushiriki Syria katika operesheni ya kumuua Abu Bakr al-Baghdadi ni uongo wa wazi, kwani Damascus haiamini Washington katu na hilo ni jambo linaloizuia nchi hiyo isishirikiane na dola hilo la Kimagharibi katika jambo lolote likiwemo suala la vita dhidi ya ugaidi. Rais Assad amesema kuhusiana na hilo kwamba: Syria haikuhusika kwa namna yoyote ile na operesheni hiyo na hakuna ushirikiano wowote ule baina ya Damascus na asasi yoyote ile ya Marekani.
Nukta ya nne na ya mwisho ni kuwa, Marekani haina nia ya kupambana na ugaidi nchini Syria, bali inachofuatilia ni mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa muktadha huo, Rais Assad amempiga kijembe Trump kwa kumtaja kuwa ‘Rais bora kabisa wa Marekani’. Rais Assad amesema: Trump ndiye Rais bora kabisa wa Marekani kwa sababu ni muwazi ukilinganisha na Marais wengine waliowahi kuitawala nchi hiyo; kwani anasema wazi na bayana kabisa kwamba, tunachokitaka sisi nchini Syria ni mafuta ya nchi hiyo, na huu ndiyo ule ukweli ulioko katika siasa za Washington.
/129