9 Desemba 2019 - 08:08
Serikali ya muda ya Libya yaeleza wasiwasi wake kuhusu mapatano ya Sarraj na Erdogan

Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya muda yenye makao yake mashariki mwa Libya amesema kuwa wanatiwa wasiwasi na mapatano yaliyofikiwa kati ya serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo yenye makao makuu yake mjini Tripoli, na Uturuki.

(ABNA24.com) Abdulhadi al Haweij Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya muda ya Libya yenye makao yake mashariki mwa nchi ambayo inaungwa mkono na wanamgambo wanaoongozwa na kamanda Khalifa Haftar, kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya amesema kuwa wanatiwa wasiwasi na mapatano yaliyofikiwa huko Tripoli kati ya Uturuki na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoongozwa na Fayez al Sarraj. Amesema kuwa kuna wasiwasi kwamba Uturuki itakabidhiwa utajiri wa taifa la Libya.

Al Haweiji aidha amesisitiza kuhusu ulazima wa kuanza mazungumzo mapana chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuunda serikali ambayo itaweza kuyapatia ufumbuzi masuala muhimu na kupambana na vitendo vya uchupaji mipaka na ugaidi.

Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki hivi karibuni alisaini hati mbili za mapatano na Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya kuhusu suala la kushirikiana katika nyanja za usalama na kijeshi na kuainisha maeneo nyeti katika bahari ya Mediterania.  

Afisa huyo wa serikali ya muda ya Libya amebainisha wasiwasi huo huku wanamgambo wenye mfungamano na kamanda muasi Khalifa Haftar wakiwa wameanzisha duru mpya ya machafuko tangu mwezi Aprili mwaka huu katika juhudi za kuudhibiti mji mkuu Tripoli.

...........
340