Rais mteule wa Iran Masoud Pezeshkian atachukua usukani wa kuongoza serikali ya awamu ya 14 huku uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za eneo ukiwa katika hali nzuri na ya kuridhisha.
Moja ya mafanikio muhimu ya serikali ya 13 chini ya uongozi wa shahidi Ebrahim Raisi ni kurejesha uhusiano na Saudi Arabia na kuboresha uhusiano na baadhi ya nchi nyingine za Kiarabu. Uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia ulikatwa mwaka 2016, na kwa sababu hiyo, nchi nyingine kadhaa za Kiarabu nazo zikaamua kuifuata Saudia kuvunja uhusiano na Iran. Mnamo Machi 2023, uhusiano huu ulirejeshwa na kuendelea kupanuka siiku baada ya siku.
Hivi sasa nchi za Kiarabu, ikiwemo Saudi Arabia, zinatarajia kuwa uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utaimarika na kupanuka pia katika kipindi serikali ya awamu ya 14 chini ya uongozi wa Pezeshkian. Kuhusiana na hilo, katika jumbe zao tofauti, mfalme na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia wamempongeza Masoud Pezeshkian kwa ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa Iran.Katika ujumbe wake wa pongezi kwa Masoud Pezeshkian, mfalme wa Saudia Salman bin Abdul Aziz Aal Saud amesema: Tuna hamu na shauku ya kupanuliwa na kustawishwa zaidi uhusiano wa nchi mbili na ndugu zetu Iran na kuendelezwa uratibu na mashauriano kwa minajili ya kuinua kiwango cha usalama na amani ya eneo na kimataifa kwa ujumla. Kwa upande wake Muhammad bin Salma mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia amesema katika ujumbe wake kwa Rais mteule wa Iran ambapo amemhutubu Masoud Pezeshkian kwa kusema kwamba: Kwa mnasaba wa ushindi wa wako katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, natumia fursa hii kukupongeza kwa dhati na ninakutakia mafanikio na maendeleo zaidi kwa ajili ya nchi na taifa ndugu. Tunasisitiza nia yetu ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili.
Kwa kutilia maanani kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi Masoud Pezeshkian alisisitiza juu ya kuchukua hatua za kustawisha uhusiano na nchi mbalimbali, inaonekana kuwa, serikali ya awamu ya 14 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendeleza kwa umakini mkakati na stratijia ya serikali ya shahidi Raisi ya kupanua uhusiano na majirani na nchi za Kiislamu. Kwa kuzingatia hili, inaweza kusemwa kuwa, ujumbe muhimu zaidi wa kuchaguliwa kwa Masoud Pezeshkian kama rais mpya kwa nchi jirani ni maudhui hii hii.
Fauka ya hayo, msingi uliowekwa na shahidi Raisi na shahidi Hussein Amir-Abdollahian kwa ajili ya kupanua uhusiano na nchi jirani unazifanya baadhi ya nchi jirani kutozingatia kustawisha uhusiano na nchi za Magharibi na Mashariki kwani hakuendani na maslahi yao, kama ilivyokuwa katika baadhi ya vipindi vingine vya urais nchini Iran. Wakati huo huo, siasa za nje za nchi za eneo la Asia Magharibi pia zimetoka katika hali ya upande mmoja na kuwa tegemezi kwa Marekani, na nchi hizi pia zimechagua kukuza uhusiano na nchi za Mashariki, hususan Russia na China kama kipaumbele katika sera zao za kigeni. Kwa hivyo, inaweza kutarajiwa kuwa, uhusiano na nchi jirani hautaathiriwa na mambo ya nje katika serikali ya awamu ya 14 ya Iran. Nukta ya mwisho ni kuwa, serikali ya awamu ya 14 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayoongozwa na Masoud Pezeshkian sambamba na kukaribisha kustawishwa uhusiano na nchi jirani na eneo hili na kwamba, itafuatilia kwa dhati suala hilo, inatarajia kuwa kupanuliwa uhusiano wa kisiasa kutaambatana pia na kustawisha uhusiano wa kiuchumi.
342/