Main Title

source : Pars Today
Jumatano

12 Juni 2019

09:05:33
950158

FAO: Mamilioni ya watoto wanatumikishwa kwenye kilimo duniani

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO limesema bado watoto wanaendelea kutumikishwa kwenye sekta ya kilimo ulimwenguni kote na hivyo kuathiri uwezo wao wa kustawi na kujinasua kwenye umaskini pindi wanapokuwa watu wazima.




Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO limesema bado watoto wanaendelea kutumikishwa kwenye sekta ya kilimo ulimwenguni kote na hivyo kuathiri uwezo wao wa kustawi na kujinasua kwenye umaskini pindi wanapokuwa watu wazima.

FAO inasema kuwa duniani kote watoto milioni 108 wa kike na wa kiume wanatumikishwa ambapo asilimia 70 wanafanya kazi kwenye sekta za kilimo, ufugaji, misitu, uvuvi na ufugaji wa samaki.

Idadi hiyo, kwa mujibu wa FAO imeongezeka kwa watoto milioni 10 tangu mwaka 2012, licha ya jitihada za Umoja wa Mataifa za kutokomeza utumikishaji watoto kwenye sekta hizo.

Ariane Genthon ambaye anahusika na programu ya FAO ya kuondokana na utumikishwaji wa watoto kwenye kilimo anasema sababu kubwa ni umaskini kwenye familia ambao husababisha wazazi kutumia watoto wao kufanya kazi kwenye kilimo.

Amesema watoto wanapotumikishwa kwenye kilimo wanashindwa kwenda shule, na hata pale wanapokwenda wanakuwa wamechoka na wanashindwa kusoma ipasavyo kama wenzao ambao hawaendi kwenye kilimo.

Bi. Genthon amesema pamoja na uchovu, watoto wanakuwa wanakumbwa na madhara ya kiafya kutokana na kemikali zinazotumika kwenye sekta ya kilimo na mara nyingi wazazi hutumia watoto wao kwa kuwa wanafanya kazi bila ujira.

Kwa mantiki hiyo amesema FAO wanasisitiza programu ya kuimarisha maeneo ya vijijini ili yawe na uwezo wa kuzalisha chakula na kushiriki kilimo bila kutumia watoto kwenye sekta ya kilimo.

Halikadhalika miradi ya kutokomeza umaskini inayolenga familia maskini ili angalau zipate kipato bila kutumikisha watoto wao.



/129