Main Title

source : Pars Today
Jumapili

30 Juni 2019

10:34:05
956347

Hitilafu za Marekani na wanachama wa G20 zagubika mkutano wa kundi hilo, Japan

Viongozi wa nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani wanakutana leo katika mji wa Osaka nchini Japan huku wingu kubwa la hitilafu na mivutano kati ya Marekani na baadhi ya wanachama wa kundi hilo likigubika ajenda ya mkutano huo.

(ABNA24.com)  Viongozi wa nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani wanakutana leo katika mji wa Osaka nchini Japan huku wingu kubwa la hitilafu na mivutano kati ya Marekani na baadhi ya wanachama wa kundi hilo likigubika ajenda ya mkutano huo.

Katika  mkondo huo maafisa wa serikali ya Japan wametangaza kuwa, hawatafanya mazungumzo na Marekani kuhusu suala la kutazama upya makubaliano ya usalama. Msemaji wa serikali ya Japan, Yoshihide Suga amesema kuwa, maafisa wa Japan na Marekani hawatafanya mazungumzo ya kutazama upya makubaliano ya kiusalama. Matamshi hayo yametolewa kujibu maneno yaliyosemwa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani ambaye alikosoa makubaliano ya kiusalama ya nchi yake na Japan na kusema, iwapo Marekani itashambuliwa, kazi pekee itakayofanywa na Wajapani ni kuketi chini na kutazama picha za mashambulizi hayo katika runinga za Sony. Trump ametaka kutazamwa upya makubaliano hayo na kudai kuwa, nchi zote ikiwemo Japan zinafaidika kwa kufanya biashara na Marekani na kwamba Tokyo na Washington zimo katika mazungumzo magumu ya kibiashara.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, hitilafu za Marekani haziishii kwa nchi mwenyeji wa mkutano wa G20 huko Osaka yaani Japan. Vitisho vipya vya Rais wa Marekani vya kuongeza ushuru wa forodha wa dola bilioni 300 kwa bidhaa za China zinazoingizwa nchini humo iwapo mazungumzo yake na mwenzake wa China hayatakuwa na matunda huko Japan na vilevile hatua ya Trump ya kuitaka India ifute ushuru mpya wa forodha dhidi ya baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka Marekani ni vielelezo vya mivutano inayoendelea kupanuka zaidi ya serikali ya Washington na wanachama wenzake katika G20.

Sababu kuu ya hitilafu hizo ni siasa za serikali ya sasa ya Marekani ambayo imeufanya uchumi wa dunia ukumbane na changamoto nyingi na kuyumbayumba kutokana na kupuuza kwake kanuni na sheria za kimataifa katika medani ya biashara na siasa za nje. 

Kuendelea mivutano ya kibiashara na kisiasa baina ya Marekani na China ambayo ndiyo uchumi wa pili mkubwa zaidi duniani, na vilevile hitilafu za Washington na wanachama wa Umoja wa Ulaya na hali kadhalika chumi zinazochipukia kwa kasi kama za India, Mexico na Brazil kunathibitisha ukweli kwamba, katika mkutano wao unaoanza leo huko Osaka, wanachama wa G20 watakuwa na mjadala mkali na mgumu kwa ajili ya kuondoa vizuizi vilivyopo vya kibiashara na kuelekeza uchumi wa dunia katika njia sahihi.

Mtandao wa habari wa NHK wa Japan umeandika kuwa: "Viongozi wa nchi wanachama katika G20 watakuwa na maudhui nguvu sana za kujadili katika kikao chao kinachoanza leo Ijumaa mjini Osaka. Viongozi hao wako chini ya mashinikizo makubwa katika kipindi cha sasa ambapo mivutano ya kibiashara na kisiasa imeshadidi. Mkutano huu unafanyika wakati wa msuguano mkali baina ya Marekani na China juu ya suala la uchumi wa dunia."

Japokuwa maamuzi ya mkutano wa G20 hayazifungi wala kuziwajibisha lolote nchi wanachama, lakini unapewa mazingatio makubwa kwa kutilia maanani kuwa, unajumuisha chumi 20 kubwa zaidi duniani ambazo zina jamii ya karibu thuluthi mbili ya watu wa dunia na zaidi ya asilimia 80 ya uzalishaji ghafi wa dunia nzima. Pamoja na hayo suala ambalo liko wazi ni kwamba, mkutano wa mwaka huu wa G20 japokuwa unafanyika nchini Japan kwa mara ya kwanza lakini kutokana na msimamo wa serikali ya sasa ya Marekani wa kung'ang'ania siasa zake za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kupuuza mitazamo ya pande nyingine, unaonekana kama hautaweza kutatua lolote kati ya mivutano na matatizo yaliyopo duniani.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Nick Robertson mwandishi na mchambuzi wa televisheni ya CNN akautaja mkutano wa G20 huko Osaka kuwa ni uwanja wa mpambano baina ya Donald Trump na nchi zinazosisitiza ushirikiano wa kimataifa na zinazopinga sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. Robertson amesema: Mkutano wa Osaka ni mpambano wa kwanza baina ya Trump na kambi ya nchi zinazopinga sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika masuala ya biashara hususan marekebisho katika Shirika la Biashara Duniani na vilevile katika suala la ustawi endelevu yaani masuala yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Alaa Kulli hal, hitilafu kubwa zilizopo kati ya nchi wanachama wa G20 na Marekani katika nyanja mbalimbali ni kielelezo kwamba, Japan ambayo ni mwenyeji wa viongozi wa G20, inakabiliana na changamoto na matatizo mengi kwa ajili ya kusimamia mkutano wenye mafanikio na matokeo ya kuridhisha.     



/129