26 Aprili 2020 - 14:12
Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yapinga mpango wa EU wa kuzuia kuingizwa silaha nchini humo

Vita vya ndani nchini Libya vilivyoanza baada ya kung'olewa madarakati dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi vimeshika mwelekeo unaotia wasiwasi mkubwa zaidi tangu Aprili mwaka jana 2019 kufuatilia mashambulizi ya wapiganaji wa linalojiita jeshi la taifa la Libya chini ya uongozi wa Khalifa Haftar, lengo likiwa ni kuudhibiti mji mkuu, Tripoli na kuing'oa madarakani Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

(ABNA24.com) Hivi sasa Umoja wa Ulaya unafanya jitihada za kuhitimisha hali hiyo kwa kuzuia kutumwa silaha huko Libya kwa pande zinazozozana.

Pamoja na hali hiyo, Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imepinga mpanbo huo wa Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa yenye makao yake makuu mashariki mwa nchi Fayez al Sarraj  Alhamisi usiku Aprili 23 aliliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akitangaza upinzani wake dhidi ya mpango huo wa Umoja wa Ulaya wa kusimamia marufuku ya kuingiza silaha nchini Libya. Al Sarraj amesema: Kama ilivyobainishwa katika azimio la Baraza la Usalama, hakuna mashauriano yoyote yaliyofanywa na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya kuhusu mpango huo. Kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ya mwezi Machi mwaka huu, UN ilipendekeza kiundwe kikosi cha usimamizi cha baharini kwa ajili ya kuisaidia serikali halali ya Libya kukabiliana uingizwaji wa silaha na kuuza nje ya nchi mafuta ya nchi hiyo kinyume cha sheria.

Wakati huo huo Josep Borrell Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza ulazima wa kusitishwa mapigano, kuhitimishwa uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya Libya na kufanyika juhudi za kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo iliyokumbwa na mgogoro. Borell ametilia mkazo ulazima wa kuanza oparesheni za majini za majeshi ya Ulaya kandokando ya Libya. Umoja wa Ulaya unatambua kuwa  vita vya ndani huko Livya ni tishio la moja kwa moja kwa maslahi ya umoja huo. Borrell amesema kuwa: Umoja wa Ulaya ikiwa taasisi ya msaada muhimu wa kuzuia kumiminika silaha nchini Libya na kuandaa mazingira ya kufikiwa mwafaka wa kidiplomasia kuhusu mgogoro wa nchi hiyo, tayari umeanzisha oparesheni mpya ya baharini huko Meditarenia ya kati.  

Umoja wa Ulaya unasimamia utekelezaji wa vikwazo vya silaha vya Libya kwa njia za anga, satalaiti na bahari kupitia oparesheni yake hiyo mpya iliyopewa jina la "IRINI".

Lengo la oparesheni hiyo limetajwa kuwa ni kurejesha utulivu nchini Libya na kusaidia mchakato wa amani unaungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Oparesheni hii mpya imechukua nafasi ya oparesheni ya baharini ya awali ya Umoja wa Ulaya katika Bahari ya Mediterania iliyojulikana kwa jina la "Sophia" ambayo ilimalizika Machi 31 mwaka huu.

Borrell ambaye mara kadhaa ametahadharisha kuhusu uingiliaji wa nchi za nje katika vita huko Libya ameeleza kuwa: "Kitendo cha kutuma silaha na zana nyingine za kijeshi nchini Libya kutoka nje ambacho ni ukiukaji wa moja kwa moja wa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa, kichochea moto wa vita nchini humo.  

Libya iligawanyika katika sehemu mbili baada ya kung'olewa madarakani utawala wa Gaddafi. Eneo la magharibi mwa nchi hiyo ambalo makao yake makuu ni Tripoli linadhibitiwa na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj ambayo imeidhinishwa na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa; na eneo la mashariki na kusini linadhibitiwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar. Mapigano ya ndani nchini Libya yameingia katika awamu mpya katika siku za karibuni kutokana na mashambulizi yanayofanywa na wapiganaji wa Haftar kwa shabaha ya kuudhibiti mji mkuu, Tripoli na kuiondoa madarakani Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya nchi hiyo.

Hata hivyo na licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Umoja wa Mataifa na ahadi zilizotolewa na mahasimu wa Libya katika mkutano wa Belin mwezi Januari mwaka huu na pia pande za kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya kwamba zitafanya juhudi za kufanikisha makubaliano ya kusimamisha vita, lakini vita vya ndani nchini humo vingali vinaendelea.

Umoja wa Mataifa sasa unataka kamati ya pamoja ya pande hizo tatu itekeleza usitishaji vita kwa kuzingatia maambukizi ya virsi vya corona. Pamoja na hayo yote, vita vya ndani vingali vinaendelea huko Livya kutokana na himaya na misaada ya silaha inayoendelea kutolewa na nchi za kigeni kwa pande mbili zinazozozana.Ukweli kwamba vita vya sasa vya kuwania madaraka huko Libya kati ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa na wanamgambo wanaoongozwa na Khalifa Haftar vinaendelea kutokana na misaada ya silaha ya nchi za kigeni kwa makundi hasimu. Kwa msingi huo hatua ya kwanza ya kweli inayopasa kuchukuliwa ili kupunguza mapigano yanayoendelea ni kusitisha kutuma silaha kwa pande zinazozozana, kutekeleza usitishaji vita na mwishowe kuanza mazungumzo ya kisiasa ili kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

..............
340