Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa iliyotolewa na ikulu ya rais wa Afghanistan imesema kuwa, katika katika hotuba yake wa washiriki wa kikao hicho cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya NAM, Rais Ashraf Ghani alisema kuwa kundi la Taleban ni lazima likubali pendekezo la usitishaji vita wa kibinaadamu ambalo limetolewa na serikali ya Kabul, kama ambavyo amezitaka nchi zote wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM kulishinikiza kundi la Taleban kukubali pendekezo hilo. Aidha rais wa Afghanistan amezitaka nchi wanachama wa NAM zilishinikize kundi la Taleban lisitishe mashambulizi yake na kujiunga na mchakato wa kisiasa ili kuweza kurejesha usalama na uthabiti nchini humo na katika eneo. Kabla ya hapo pia Rais Muhammad Ashraf Ghani alikuwa amelitaka kundi hilo likubali pendekezo la usitishaji vita, hata hivyo Taleban ilikataa. Ombi la rais Ghani kwa Kundi la Mawasiliano la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya NAM la kulitaka lilishinikize kundi la Taleban likubali mpango wa usitishaji vita nchini Afghanistan, linabainisha kufeli Marekani katika kulishawishi kundi hilo liweze kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya baina ya Waafghani ili kufikiwa mapatano ya usitishaji vita wa kudumu. Marekani ambayo baada ya kutia saini makubaliano ya amani na kundi la Taleban hapo tarehe 29 Februari mwaka huu mjini Doha, Qatar iliyataja makubaliano hayo kuwa ni mafanikio yake makubwa dhidi ya kushindwa kwake kikamilifu katika vita vya Afghanistan, sasa imefeli kuendelea kulishawishi kundi hilo liweze kushiriki mazungumzo kati ya Waafghani; na kimsingi White House imegeuka na kuwa mshiriki asiye na taathira yoyote katika matukio ya nchi hiyo ya Asia.
Kupitia ahadi zake za kuondoka Afghanistan, Marekani iliweza kulishawishi kundi la Taleban kutia saini mapatano ya amani ya mjini Doha, hata hivyo katika kipindi kinachokaribia miezi miwili iliyopita Washington haikchukua hatua yoyote ya maana ya utekelezaji wa makubaliano hayo na ni kwa msingi huo ndipo kundi hilo likaituhumu mara kadhaa White House kuwa imekiuka ahadi zake pamoja na kufanya hadaa. Hasa kwa kuzingatia kuwa serikali ya Marekani hadi sasa bado haijaweka wazi muda maalumu wa kuondoa kikamilifu askari wake kutoka Afghanistan kwa mujibu wa mapatano ya mjini Doha, suala ambalo iwapo Washington haitolitekeleza, basi itakabiliwa na radiamali kali ya kundi hilo. Aidha katika mapatano ya nchini Qatar serikali ya Marekani ilitoa ahadi kwa niaba ya serikali ya Afghanistan tena bila kuwepo mawasiliano na nchi hiyo ya kuachiliwa huru wafungwa wa Taleban kabla ya kufanyika mazungumzo kati ya Waafghani, jambo ambalo kutekelezwa kwake kama ilivyotarajiwa na kundi hilo, ni kwenda kinyume na maslahi na usalama wa taifa la Afghanistan. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afghanistan sambamba na kuchukua uamuzi wa kuwaachilia huru hatua kwa hatua wafungwa wa Taleban, amejitahidi kuifanya njia hiyo kuwa ni kipimo cha kufungamana kundi hilo na ahadi zake za kupunguza mashambulizi nchini humo. Hatua hiyo ya matiki pia imeungwa mkono na raia na makundi ya kisiasa ya Afghanistan.
Kwa kuzingatia kuwa ahadi za Marekani katika mapatano yake na kundi la Taleban zimeisababishia changamoto kubwa serikali ya Kabul kwenye mwenendo wa mazungumzo kati ya Waafghani, hivi sasa viongozi wa Afghanistan wanakusudia kutumia njia mbadala za kieneo na kimataifa kwa ajili ya kusaidia kwenye kupatikana usitishaji vita ndani ya nchi hiyo. Katika mazingira hayo ndipo kwenye kikao cha Kundi la Mawasiliano la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afghanistan akazitaka nchi hizo zilishinikize kundi la Taleban likubali pendekezo la usitishaji vita wa kibinaadamu lililotolewa na serikali ya Kabul. Inaonekana kwamba hivi sasa hatua pekee inayoweza kulifanya kundi la Taleban kuingia kwenye mwenendo wa mazungumzo kati ya Waafghani, mbali na kulivutia kwenye mapatano ya kuhitimisha vita na usitishaji vita wa kudumu, ni kuonekana irada ya dhati katika mpango wa Marekani wa kuondoka kikamilifu Afghanistan; na pande nyingine kama Kundi la Mawasiliano la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM haziwezi kutoa mchango athirifu kwenye ulingo wa matukio ya amani ya nchi hiyo ya Asia.
342/