16 Mei 2020 - 10:05
Radiamali ya Rais wa Afghanistan kwa shambulio la kigaidi dhidi ya Wodi ya Wazazi mjini Kabul

Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afghanistan ametoa radiamali yake kwa shambulio la kigaidi dhidi ya hospitali moja katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul na kusema kwamba, sehemu yoyote ya wananchi wa Afghanistan inapolengwa na shambulio basi yeye hujihesabu kuwa anatokea katika eneo hilo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA:Akikagua hospitali hiyo iliyolengwa kwa shambulio la kigaidi, Rais Ashraf Ghani amesema kuwa, wananchi wa Afghanistan ni taifa moja na hakuna Muafghani ambaye ni bora kuliko mwenzake. Ashraf Ghani ameongeza kuwa, kama makundi ya kigaidi yanadhani kwamba, yanaweza kuleta hitilafu na mifarakano baina ya wananchi wa nchi hiyo kupitia mashambulio hayo yanajidanganya na hayatafikia lengo lao hilo.

Rais wa Afghanistan ameashiria amri aliyoitoa kwa vikosi vya ulinzi na usalama ya kujiondoa katika hali ya kujihami na kujiweka katika hali ya kushambulia kwa ajili ya kukabiliana na kundi la wanamgambo wa Taliban na kuongeza kuwa, shambulio dhidi ya hospitali ni kinyume kabisa na maamrisho ya dini tukufu ya Kiislamu na hatua hiyo inaonyesha ukatili, jinai na upotovu walionao watekelezaji wa shambulio hilo ambapo hiyo ni dhambi isiyo na msamaha.

Shambulio la kigaidi dhidi ya Kitengo cha Wodi ya Wazazi katika hospitali moja ya mji mkuu Kabul ambalo kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika kwake, kwa mara nyingine tena limeonyesha kuwa, Afghanistan inakabiliwa na aina mbalimbali ya makundi ya kigaidi; na hata makubaliano tarajiwa ya amani baina ya serikali na Taliban hayawezi kuhitimisha vita na vitendo vya utumiaji mabavu katika nchi hiyo.

Tarehe 29 ya mwezi Februari mwaka huu kundi la Taliban na Marekani zilitiliana saini katika mji mkuu wa Qatar, Doha makubaliano ya amani ambapo wanamgambo hao waliahidi kupunguza machafuko. Baada ya kutiwa saini makubaliano hayo, serikali na wananchi wa Afghanistan walipata matumaini kwamba, kwa akali machafuko ambayo chimbuko lake ni Taliban yatapungua na hatua kwa hatua yatasitishwa. Hata hivyo kivitendo hilo halijafanyika, na hata karibuni hivi kundi la Taliban limetishia kushadidisha mashambulio yake.

Matukio ya miezi ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa, makubaliano ya Marekani na wanamgambo wa Taliban siyo tu kwamba, hayajasaidia kupunguza machafuko na vitendo vya utumiaji mbavu nchini Afghanistan, bali yamezifanya juhudi za serikali ya Kabul za kurejesha amani na uthabiti zikabiliwe na changamoto mpya. Shambulio la hivi karibuni la Daesh dhidi ya hospitali moja ya wanawake mjini Kabul limedhihirisha kuwa, kutokana na Afghanistan kukabiliwa na vitisho vya aina mbalimbali ina kibarua kigumu kwa ajili ya kudhamini amani na usalama.

Kwa muktadha huo, serikali ya Kabul haipaswi kutumia nguvu zake zote kwa ajili ya kutaka amani na Taliban, bali sambamba na hilo inapaswa kutumia pia nguvu zake katika kukabiliana na makundi mengine ya kigaidi pamoja na vitisho vyao angamizi.

Atiqullah Amirkhil, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Afghanistan anasema: Kabla ya kufikiwa makubaliano ya amani na Taliban, kundi la kigaidi la Daesh linapaswa kusambaratishwa kwanza, kwani baada ya kufikiwa makubaliano tarajiwa, kundi hili litapata nguvu.

Licha ya kuwa, miezi kadhaa iliyopita Hamdullah Mohib mshauri wa usalama wa taifa wa Rais Afghanistan hakuliona kundi la Daesh kama tishio la kiistratejia kwa nchi hiyo, lakini kundi hilo limeonyesha kuwa, linaweza kutoa changamoto kubwa kwa suala la kudhamini usalama nchini humo hata baada ya kufikiwa makubaliano tarajiwa baina ya serikali ya Kabul na wanamgambo wa Taliban.

Msimamo wa Hamdullah Mohib aliutangaza katika kipindi ambacho, Baraza la Usalama wa Taifa la Afghanistan lilitoa wito wa kuweko juhudi za pamoja za kimataifa za kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh, ambapo takwa kama hilo lilionyesha wazi kuwa, baraza hilo linaamini kwamba, kundi hilo ni tishio la kiistratejia kwa ajili ya kudhamini usalama wa taifa wa nchi hiyo. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kuhusiana na mauaji ya raia nchini Afghanistan na kueleza kuwa, asilimia 52 ya raia wa nchi hiyo waliuawa kwa mashambulio ya kigaidi ya Daesh ambapo idadi kubwa zaidi ya mauaji hayo ilishuhudiwa katika mji mkuu Kabul na Nangarhar.