21 Mei 2020 - 13:04
Takht-Ravanchi: Hotuba ya Kiongozi Muadhamu itapelekea kuangaziwa kadhia ya Palestina duniani

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu katika Umoja wa Mataifa amesema hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Siku ya Kimataifa ya Quds itaigeuza kadhia ya Palestina kuwa kadhia nambari moja duniani kinyume na jitihada zinazofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Majid Takht-Ravanchi,Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyasema hayo Alhamisi katika mahojiano na Shirika rasmi la Habari la Iran, IRNA.

Ameongeza kuwa, wakati huu wa kujadiliwa maudhui za 'Muamala wa Karne' na  kuuganishwa maeneo zaidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (yaani Israel), hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Siku ya Kimataifa ya Quds itaweka wazi msimamo wa Iran na ulimwengu wa Kiislamu kuhusu kadhia ya Palestina na Quds na hivyo kuweza kuifanya jamii ya kimataifa izingatie zaidi kadhia hiyo.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu katika Umoja wa Mataifa amesema utawala ghasibu wa Israel umepora na kunyakua ardhi za jadi za Wapalestina na kuwafanya wawe wakimbizi na hii ni nukta ambayo watu wote duniani wanapaswa kuifahamu. Aidha amesema kuna haja ya kufanyika jitihada za kuhakikisha kuwa, jamii ya kimataifa inapaza sauti moja ya kukabiliana na ukandamizaji na dhulma wanazotendewa watu wa Palestina.

Takht-Ravanchi amesisitiza kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds na mshikamano wa kimataifa wa ulimwengu wa Kiislamu na wapenda uhuru duniani katika kuwatetea watu wa Palestina ni jambo ambalo litakuwa na mchango mkubwa katika kufikiwa malengo matukufu ya Palestina.

Kesho Ijumaa tarehe 22 Mei 2020 sawa na 28 Ramadhani 1441 itakuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei anatazamiwa kutoa hotuba muhimu.