7 Juni 2020 - 08:20
Rais Rouhani: Watu wa afya daima wamekuwa wakipata mafanikio ya kujivunia nchini Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia mafanikio waliyoyapata watu wa afya humu nchini katika masuala ya kisayansi na utafiti wa kupambana na kirusi cha corona na kusema, watu wa fya nchini Iran daima wamekuwa wakipata mafanikio ya kujivunia.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumamosi katika kikao cha Kamati ya Taifa ya Kupambana na Corona na kuongeza kuwa, katika upande wa maendeleo ya kielimu, Iran inashika nafasi ya 15 kote ulimwenguni na kwa upande wa eneo la Asia Magharibi na ulimwengu wa Kiislamu inashika nafasi ya kwanza.

Aidha amesema, madaktari, wauguzi na watu wote wa afya nchini Iran ni wapambanaji imara katika medani ya afya na kusisitiza kuwa, kudhaminiwa mahitaji ya tiba na matibabu kwa ajili ya kupambana na corona, kutoa huduma za dharura kwa jamii, kudhamini vitu vya dharura na vya kimsingi na kutolewa fedha na misaada maalumu ya kuwasaidia watu wenye shida ni majukumu manne muhimu zaidi ya serikali yake ambayo yametekelezwa vizuri katika kipindi chote hichi.

Rais wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran amegusia pia kugunduliwa dawa mbili zenye taathira kubwa na zinazotia matumaini mazuri sana ya kutibu ugonjwa wa corona nchini Iran na kusema, wiki hii, shughuli za tiba na matibabu humu nchini zimeingia kwenye awamu yake ya tatu ya kupambana na corona ambayo ni ya kuzingatia zaidi watu wanaoweza kuathiriwa mno na COVID-19.

Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa wagonjwa laki moja na 38,132 wameshapona ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Hadi hivi sasa watu wote waliogunduliwa kuwa na ugonjwa huo humu nchini ni Laki moja na 69,425. Sampuli milioni moja na 60 elfu zimeshafanyiwa uchunguzi wa corona hadi hivi sasa nchini Iran.

Watu wote waliokumbwa na COVID-19 hadi leo Jumamosi kote duniani ni zaidi ya milioni 6 na laki nane na 70 elfu. Marekani ndiyo inayoongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa na watu waliofariki dunia kwa corona. Uingereza inaifuatia Marekani kwa idadi kubwa zaidi ya vifo vya ugonjwa wa COVID-19.

342/