2 Agosti 2020 - 10:29
Palestina yalaani mpango wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Quds

Serikali ya Palestina imelaani hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kupasisha mpango wa ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni huko kaskazini mwa mji wa Quds (Jerusalem).

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Palestina imesema kuwa, uamuzi huo wa kujenga vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Quds ni sehemu ya mpango wa Israel wa kutwaa kikamilifu eneo la Quds, kubadilisha sura yake ya kihistoria na kuharibu kabisa utambulisho wake wa Kipalestina.

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Palestina imeitaka jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake mkabala wa harakati hizo za Wazayuni wa Israel na imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kufanya uchunguzi wa haraka juu ya jinai zinazofanywa na Israel na kuwachukulia hatua viongozi husika wa utawala huo.

Televisheni ya Israel ilitangaza jana Jumamosi kwamba mamlaka ya mji wa Quds imeafiki mpango uliopasishwa na Wizara ya Masuala ya Quds wa kujenga kitongoji kipya huko kaskazini mwa mji huo mtakatifu.

Harakati hizi za Israel zinatajwa kuwa ni sehemu ya mpango wa "Muamala wa Karne" uliobuniwa na Rais Donald Trump wa Marekani ambao umepingwa vikali na harakati na vyama yote vya Palestina.

Mpango huo unasisitiza kuwa eneo lote la Quds (Jerusalem) Mashariki na Magharibi ni mji mkuu wa Israel, kinyume kabisa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo mabalozi wa nchi 15 za Ulaya wamewaandikia barua viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakipinga ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.

342/